Mtizamo wa kiuchumi zuio la mifuko ya plastiki

Thursday April 18 2019

 

By Honest Ngowi

Serikali imeweka msimamo wa kuondoa mifuko ya plastiki kuanzia Juni Mosi. Hili ni miongoni mwa maagizo yaliyoleta mjadala mkubwa hivi karibuni.

Tangazo la zuio hilo limetolewa bungeni na Waziri Mkuu, Kasim Majaliwa. Sababu iliyotolewa ni athari za mifuko hiyo kwenye mazingira kutokana na ukweli kwamba mifuko hii haiozi kiurahisi.

Kuna mitizamo tofauti ya kiuchumi ya kuhusu katazo hili. Kwanza ni athari mbalimbali za kimazingira zinazotokana na shughuli mbalimbali za binadamu ambazo zinahusisha uzalishaji, usafirishaji, uhifadhi, utumiaji na utupaji wa bidhaa na huduma.

Athari hizi zinatofautiana na kanuni za uchumi wa kijani unaohamasisha utunzaji wa mazingira kwa maana ya mimea na wanyama wa majini na nchikavu.

Uchumi wa kijani ni baadhi ya mikakati ya kuyafikia maendeleo endelevu ambayo yanatizama uchumi na hatma ya mazingira kwa kizazi hiki na vijavyo. Ni uchumi unaohakikisha wajukuu hawapigwi ganzi kwa kosa la mababu kula zabibu mbichi.

Ni mkakati unaojaribu kutekeleza falsafa kuwa hatukuirithi dunia kutoka kwa mababu zetu bali tumeokopa kutoka kwa watoto na watoto wa watoto wetu hivyo tutakapoondoka ni lazima tuiache ikiwa safi kuliko tulivyoikuta.

Malengo ya uchumi wa kijani ni pamoja na kuchangia kupunguza umasikini, ukuaji endelevu wa uchumi, maisha bora na fursa za ajira endelevu zenye staha kwa wote. Yote haya yanatakiwa kufanyika bila kuathiri mazingira

Fursa

Kiuchumi na kijasiriamali, katazo la kutumia mifuko ya plastiki ni fursa kwa wanaotaka kuwekeza katika uzalishaji na uuzaji wa mifuko mbadala ambayo ni rafiki kwa mazingira.

Hawa ni waliopo kwenye mnyororo wa thamani. Wanaweza kuwa wanaosanifu na wazalishaji wa mitambo na malighafi za kutengenezea mifuko hii, vyombo vya fedha, wasafirishaji na hasa watengenezaji na wauzaji wa mifuko hii.

Hata hivyo ni muhimu kukumbuka kuwa kuwepo kwa fursa kama hii ni suala moja na kuitumia vizuri ni suala jingine. Ili fursa hii isipotee ni lazima yawepo mazingira wezeshi na rafiki kwa wadau kufaidi nayo.

Mazingira haya ni pamoja na utayari wa kuwekeza katika mifuko mbadala, upatikanaji wa mitambo, mtaji fedha, vibali na kadhalika. Kwa waliopo katika biashara hii kinachohitajika kwao kwa muda mfupi uliopo hadi Juni Mosi ni utayari wao kutosheleza mahitaji ya soko kwani yataongezeka kutokana na ombwe litakaloachwa baada ya kuzuiwa iliyopo.

Changamoto

Ingawa kuna fursa, zuio hili lina changamoto pia kwa baadhi ya wadau. Waliokuwa wanazalisha mifuko ya plastiki, kama mitambo na teknolojia yao ya uzalishaji haitobadilika ili wazalishe mifuko mbadala, itakuwa ni changamoto.

Uwekezaji wao kwenye mitambo na teknolojia pamoja na akiba ya malighafi ambayo itakuwa haijatumika itakuwa ni hasara kwao. Kama itabidi kusimamisha uzalishaji itamaanisha baadhi ya watu watapoteza ajira hivyo kulazimika kutafuta chanzo kingine cha kipato halali.

Kama mitambo hii inaweza kubadilishwa na kuzalisha mifuko mbadala, changamoto itakuwa ni gharama za kuibadilisha.

Changamoto nyingine ni akiba ya mifuko iliyozalishwa lakini haijauzwa. Hii itasababisha hasara na kuyumba kifedha kwa wahusika hivyo ugumu wa kufanya marejesho kama walikopa kwenye taasisi za fedha, kulipa mishahara ya wafanyakazi na wengineo.

Mengineyo

Mifuko ya plastiki ni kati ya mambo yanayokwamisha uchumi wa kijani hivyo katazo hili ni jambo jema kwa mazingira. Hata hivyo ni lazima mambo mengine kuelekea uchumi wa kijani yaanze au yaendelee kufanyika.

Haya ni pamoja na kutoa elimu kuhusu athari za kiuchumi na mazingira machafu zitokanazo na shughuli za binadamu hivyo umuhimu wa kuwepo kwa kodi zinazotozwa ili kudhibiti uchafuzi na kusaidia usafishaji wa mazingira.

Yote haya yatafanikiwa kwa kufanya tathmini na uchambuzi wa athari za kimazingira za shughuli zote za kiuchumi. Muhimu zaidi ni kuwafundisha wadau wote hasa watoto kuhusu umuhimu wa mazingira kwa maendeleo endelevu na maisha kwa ujumla.

Advertisement