Paschal mtengeneza viatu anayejiunga kidato cha tano

Paschal Fanuel akipanga viatu vya aina tofauti anavyovitengeneza tayari kuviuza kwa wateja watakaojitokeza. Picha na Ngollo John.

Wakati kukiwa na melfu ya vijana wanaojiunga chuo kikuu bila kujua wanataka kuwa nani wakihitimu hivyo kusababisha mlundikano wao mtaani, ni tofauti na Paschal Fanuel (18).

Akiwa miongoni mwa vijana waliomaliza kidato cha nne, Paschal tayari anao ujuzi wa kutengeneza viatu na anachopanga ni kuongeza maarifa yatakayomsaidia kumiliki kiwanda cha bidhaa za ngozi.

Mhitimu huyu wa Sekondari ya Mhandu iliyopo jijini Mwanza anasema alianza kushona viatu tangu akiwa darasa la sita, mwaka 2013 hivyo atakapohitimu chuo kikuu miaka kadhaa ijayo, ataendelea kuifanya shughuli hiyo.

Akizungumza na gazeti hili anasema alipata maarifa hayo baada ya kuhudhuria mafunzo ya ujasiriamali yanayotolewa na shirika la dini la Compassion lililo chini ya makanisa 12 ya kiinjilisiti ya jijini Mwanza. “Haikuwa ndoto yangu kujifunza utengenezaji wa viatu kwani tangu nikiwa mtoto nilitamani zaidi kuwa daktari wa kutibu watu lakini Shirika la Compassion limenifanya niwe na ujuzi ninaoweza kujiajiri nitakapomaliza chuo kikuu,” anasema Paschal.

Fanuel ni wa kwanza kuzaliwa na anao ndugu watano wanaomfuata kutoka kwa baba anayejishughulisha na uashi huku mama yake mjasiriamal mdogo.

Familia yake, anasema inaishi maisha ya kawaida ila yanamtegemea sana Mungu na amelelewa katika maadili ya kidini. Yeye na wadogo zake wanasoma shule za Serikali.

Kijana huyo aliyechaguliwa kujiunga kidato cha tano kwenye moja ya sekondari zilizopo mkoani Iringa, anasema alipenda kuwa daktari na akasoma masomo ya sayansi lakini hakufaulu kiasi kukidhi vigezo vya kuendelea nayo.

Hata hivyo, baada ya kuhitimu kidato cha nne mawazo yake yamebadilika. Badala ya kufikiria udaktari, sasa anataka kuwa mwanasheria huku akiendelea kuweka nguvu kwenye ushonaji.

“Natamani nikimaliza chuo nije nimiliki kiwanda cha ushonaji viatu,” anasema kijana huyo mwenye malengo ya kuendeleza taaluma na ujasiriamali kwa wakati mmoja.

Malighafi

Mwalimu Shirika la Compassion aliyemfundisha Paschal kutengeneza viatu, Pastory Kulwa anasema upatikanaji wa malighafi ni changamoto kwa wazalishaji wadogo kwani kutokana na kutokuwa na viwanda vya kuisindika vya kutosha nchini, wanalazimika kununua kutoka Moshi au Kenya.

“Tunaiomba Serikali isaidie kufufua kiwanda cha Mwanza Tanneries ili kirahisishe upatikanaji wa ngozi na kuwapunguzia gharama za kupata,” anasema

Kwa sasa, mita moja ya mraba ya ngozi iliyochakatwa wanainunua kwa Sh3,000, gharama ambayo wanasema ni kubwa.

Licha ya ugumu wa upatikanaji wa malighafi, Kulwa anasema masoko ni changamoto nyingine wanayokabiliana nayo kwani watu wengi wanapenda bidaa kutoka nje ingawa wao wanazo mashine zote zinazohitajika kutengeneza viatu imara na vya kisasa.

“Serikali iwajali wajasiriamali wadogo kwa kulinda soko la ndani na kuhakikisha wanapata malighafi ya uhakika,” anasema Kulwa.”

Serikali

Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Dk Philis Nyimbi amepongeza juhudi za Paschal na kusema hiyo ndio dhana halisi ya uchumi wa viwanda kwani pamoja na kufanya vyema kwenye masomo yake anao ujuzi wa kujiajiri.

Dk Nyimbi alitumia mfano huo kuwataka vijana wengine kutafuta ujuzi utakaowawezesha kujiajiri hata kama wanaendelea na masomo.

“Paschal ni mmoja mabalozi tunaotakiwa kuwa nao kwenye jamii hivyo kila mmoja ahakikishe anatumia ujuzi wake kufanya jambo na si kutegemea ajira pekee,” anasema Dk Nyimbi.