Serikali inadaiwa Sh2.39 trilioni na mifuko hifadhi ya jamii

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Profesa Asad

Dar es Salaam. Deni la Serikali katika mifuko ya hifadhi ya jamii limefikia Sh2.39 trilioni, Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) imebainisha.

Ripoti hiyo iliyowasilishwa bungeni Aprili 10 imebaini mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii ina madai makubwa ambayo ni chechefu au yasiyolipika na mengi ni ya Serikali na taasisi zake.

Mpaka Juni 30, 2018, zaidi ya asilimia 68 ya madeni ya Serikali na taasisi zake yalikuwa bado hayajalipwa Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) na hadi Julai 31, 2018 kwa madeni ya LAPF, PPF, GEPF na PSPF ingawa baadhi ya mikopo ilikuwa imeiva tangu 2014.

“Hali hii inasababisha mifuko kuwa katika hali ya ukata kiasi cha kukwaza utekelezaji wa majukumu yake. Deni ambalo Serikali inadaiwa na mifuko ya hifadhi ya jamii limefika Sh2.39 trilioni,” amesema CAG.

Kwenye ripoti hiyo, Profesa Mussa Assad amebainisha madeni ya Serikali kwenye mifuko tofauti kwa mwaka 2018. Amesema LAPF inadai Sh169.64 bilioni, NSSF Sh1.25 trilioni na PPF Sh292.11 bilioni.

Vilevile, mfuko wa GEPF unadai Sh10.04 bilioni, PSPF Sh448.9 bilioni na NHIF Sh216.2 bilioni hivyo kufanya jumla ya Sh 2.39 trilioni.

Deni la NSSF pia linajumuisha kiasi cha Sh127.89 bilioni ambacho Serikali ilipaswa kuchangia katika ujenzi wa Daraja la Kigamboni.

Mkopo wa mfuko wa NHIF unajumuisha Sh 115.11 bilioni ambazo waliwapa Chuo Kikuu cha Dodoma kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha afya kwa ajili ya mafunzo. CAG anasema mkopo huu haukuwa na dhamana kutoka Serikalini wala hapakuwa na makubaliano ya kisheria.

Hata hivyo, Profesa Assad amesema ni muhimu sana kwa mikopo hii kurejeshwa kwa wakati ili mifuko iweze kujiendesha na kutimiza malengo yake, ikiwamo kulipa mafao ya wastaafu.

“Kwa ajili ya uhakika na uendelevu wa mifuko, napendekeza Serikali na Taasisi zake kulipa kiasi wanachodaiwa kwa wakati ili kuisaidia mifuko kufikia malengo yake.” Ameshauri Profesa Assad.