Ubalozi wa Tanzania nchini China unavyokuza utalii

Friday June 7 2019

 

By Mussa Juma, Mwananchi [email protected]

Katika vipaumbele vikubwa vya Serikali ni kukuza kupitia viwanda ili Tanzania iwe na uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Wakati mikakati hiyo ikiwekwa kwenye vyanzo vya ndani, kimataifa, msisitizo ni kuimarisha diplomasia ya uchumi yenye kipaumbele cha kukaribisha wawekezaji zaidi pamoja na kuongeza idadi ya watalii.

Kuonyesha kuwa haitanii katika eneo hilo, Serikali imelifufua Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na kwenye bajeti ya mwaka 2019/20, imelitengea Sh500 bilioni kwa ajili ya kuongeza ndege mpya.

Alipokuwa anazungumza na mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania kwenye mataifa tofauti duniani, Oktoba 2016 jijini Dar es Salaam, Rais John Magufuli alimtaka kila mmoja anasaidia kuvutia wawekezaji na kuvutia watalii na kuwakumbusha kuachana na kuandika ripoti za vikao wakiwa ofisini.

Rais alikumbusha kuwa, pamoja na sifa nyingine, watapimwa utendaji wao kwa uwekezaji watakaovutia kuja nchini.

Mapema mwaka 2016, aliyekuwa waziri wa maliasili na utalii, Profesa Jumanne Maghembe aliiagiza Boti ya Utalii Tanzania (TTB) kuhakikisha inaweka mikakati itakayoongeza idadi ya wageni wanaotembelea vivutio vilivyopo mpaka wafike milioni mbili mwaka 2018, lengo ambalo mpaka leo halijatimia ingawa juhudi zinaonekana.

Advertisement

Sekta ya utalii nchini imeajiri takriban watu 500,000 na wengine zaidi ya milioni moja wakijiajiri wenyewe hivyo kuchangia asilimia 17.5 katika pato la Taifa (GDP) hivyo kuwa miongoni mwa maeneo yanayochangia pakubwa kwenye uchumi.

Kutokana watalii milioni 1.1 waliokuja nchini mwaka 2015, wameongezeka mpaka karibu milioni 1.5 mwaka 2018 ambao, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inasema waliliingizia Taifa Dola 2.44 bilioni.

Mikakati

Mwaka huu, sekta ya utalii inatarajiwa kufanya vizuri zaidi dalili zikijionyesha baada ya ujio wa zaidi ya watalii 1,340 kutoka Israel na China waliotembelea hifadhi za Taifa na vivutio vilivyopo nchini.

Ujio wa watalii hawa ni matokeo ya ushirikiano baina ya Serikali, TTB, Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa), Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) na wadau wengine.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameshuhudia matokeo ya ushirikiao huo alipopokea watalii 342 Mei 12 wakiwamo wafanyabiashara na wawekezaji kutoka Zhejiang, China.

Watalii hao ni kundi la kwanza miongoni mwa 10,000 wanaotarajiwa kutembelea Tanzania mwaka huu.

Katika hafla ya kuwapokea wageni hao, Majaliwa alimshukuru mwenyekiti wa kampuni ya Touchroad International, Liehui He kwa ushirikiano anaoutoa.

“Mbali na kutuunganisha Watanzania na Wachina, tunakushukuru kwa kuamua kuitangaza Tanzania na fursa ilizonazo,” alisema Majaliwa.

Waziri mkuu pia aliwapongeza watendaji wa TTB na kampuni za kuhudumia watalii kwa mapokezi mazuri na kumpa sifa balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki kwa uratibu wa watalii hao.

Mipango

Mkurugenzi mkuu wa TTB, Devotha Mdachi anasema China ni miongoni mwa masoko ya kimkakati ya utalii kama ilivyo Israel iliyoleta watalii 1,000. Vilevile, Oman, Urusi na Australia zimo kwenye orodha hiyo pia.

Kutokana na mikakati iliyowekwa kwenye masoko hayo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangallah anasema Serikali imewekeza kutangaza vivutio vilivyopo ili kuongeza idadi ya watalii wafike zaidi ya milioni mbili hadi mwakani.

Anasema baada ya kufanyavizuri kuvutia watalii, katika nchi za Marekani, Uingereza,Ujerumani, Ufaransa na Italia sasa kazi inaendelea kufanywa katika mataifa mengine ya vipaumbele vya utalii na kujitangaza.

“Tuliwekeza Marekani, Ujerumani, Uingereza, Ufaransa na Italia ila sasa hivi uelekeo wetu ni China, Israel, Oman na nchi za ghuba, Australia na Urusi,” anasema.

China

Ongezeko la watalii kutoka China halitokei kwa bahati mbaya bali juhudi zinazofanywa na maofisa wa ubalozi wa Tanzania uliopo nchini humo.

Balozo Mbelwa anatoa mfano kuwa baada ya kutangaza vivutio jijini Hong Kong, watalii 200 watakaokaa nchini kwa siku nane wanatarajiwa kuja mwezi ujao.

“Ubalozi unakamilisha mazungumzo na kampuni ya PR Network kwa ajili ya ziara ya mcheza filamu mashuhuri wa China kutembelea Tanzania,” anasema Mbelwa.

Vilevile, wiki hii, ubalozi huo umeingia makubaliano na kituo cha runinga cha Hainan kinachotazamwa na zaidi ya watu milioni 200 kutengeneza kipindi maalumu kutangaza bidhaa, utamaduni na vivutio vya utalii vya Tanzania. Kipindi hicho kitarushwa Novemba.

Mwishoni mwa mwezi uliopita, ubalozi huo pia ulizindua matangazo ya utalii katika stesheni ya treni cha Yong’anili kilichopo jijini Beijing.

Hata hivyo, Mbelwa anasema Watanzania pia wanapewa fursa kubwa na Taifa hilo kunufaika na fursa za kibiashara zilizopo kwa kuuza bidhaa za aina tofauti.

Sasa hivi kwa mfano, amesema wapo baadhi wanaoshiriki maonyesho ya kimataifa ya bidhaa za mbogamboga na matunda (horticulture) ambayo yatadumu kwa miezi sita hadi Septemba. Mwezi uliopita, wachongaji na wachoraji sita walishiriki maonyesho ya sanaa na kuuza bidhaa zao.

“Endapo wajasiriamali wetu watajipanga, kuna fursa nyingi za kunufaika nazo nchini China ambako wanapewa nafasi ya kujitangaza na kulifikia soko la hapa ambalo ni kubwa sana,” anasema Kairuki.

Advertisement