Ukitimiza wajibu wako utadai haki zako kazini

Thursday February 28 2019Justine Kaleb

Justine Kaleb 

By Justine Kaleb

Usipojua hatima ya safari yako, unaweza kupelekwa popote nawe usijue kuwa inakuchelewesha kufanikisha malengo yako.

Huwezi kudai kitu ambacho hufahamu uwepo wake na huwa mbaya zaidi usipojua kinapatikanaje au nani anawajibika kukupatia. Kama kuna jambo la muhimu sana kwa mfanyakazi, kabla ya kazi yenyewe na mshahara atakaolipwa ni kujua haki zake na wajibu wake kisheria.

Kwa mujibu wa sheria ya ajira na uhusiano kazini ya mwaka 2004 na Sheria ya Usalama Kazini ya mwaka 2003, kila mfanyakazi anazo haki anazopaswa kuzifahamu na kuzipata.

Haki hizi ni pamoja na mkataba wa kazi, kufahamu nafasi na majukumu ya uliyoajiriwa ili usifanye majukumu yasiyokuhusu.

Mfanyakazi ana haki ya kwenda likizo isiyopungua siku 28 kwa kila mwaka, kupewa likizo ya matibabu mpaka siku 126 endapo ataugua na ya uzazi; siku 84 kwa mwanamke aliyejifungua mtoto mmoja au siku 100 kwa zaidi ya mmoja. Mwanaume hupewa siku tatu.

Mfanyakazi ana haki ya kulipwa kulingana na kazi anayofanya. Endapo ataumia akiwa kazini, ana haki ya kuhudumiwa kwa matibabu na mwajiri na kulipwa fidia ya madhara aliyoyapata kutoka Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF).

Mfanyakazi hatakiwi kubaguliwa, kunyanyaswa wala kudhalilishwa kijinsia. Yuko huru kujiunga na chama cha wafanyakazi ili kutetea masilahi yao kwa pamoja.

Mfanyakazi ana haki ya kuvunja mkataba wa kazi kwa kufuata utaratibu na endapo ataachishwa au kustaafishwa basi alipwe stahiki zinazomhusu ikiwamo malipo ya notisi, kiinua mgongo, usafiri, cheti cha utumishi, mafao ya hifadhi ya jamii, malimbikizo ya likizo na mengineyo.

Sheria pia imeweka inampa wajibu wa kutoa taarifa kwa maandishi mapema tatizo linapotokea wakati wa ugonjwa, ajali au kuibiwa. Kutoa notisi au malipo unapotaka kuacha kazi. Kutoa taarifa ya kujifungua kabla ya mwezi husika.

Kwa kufuata utaratibu wa kisheria, mfanyakazi anaweza kushiriki migomo na kutumia njia za kidiplomasia kutatua migogoro na mwajiri badala ya uvunjifu wa amani. Ni muhimu kukumbuka kila haki inaambatana na wajibu. Kabla hujadai haki zako, timiza wajibu wako kwanza.

Advertisement