Upatikanaji wa mikopo kwa vijana wajasiriamali urahisishwe kukuza ajira

Muktasari:

  • Kila biashara inahitaji mtaji hasa fedha kwa ajili ya uendeshaji wa kila siku. Vijana ni kundi lisilopewa kipaumbele kwenye taasisi nyingi za fedha jambo linalochelewesha maendeleo yao na ya jamii kwa ujumla. Wadau wanashauriwa kurahisisha masharti yaliyopo ili kuwawezesha vijana kufanikisha miradi yao na kutekeleza mawazo waliyonayo.

Vyovyote iwavyo, maisha lazima yaendelee licha ya changamoto zitakazojitokeza katika safari hiyo. Bila kujali umri, kila mmoja anayo malengo anayokusudia kuyatimiza.

Kati ya mambo yanayowakabili vijana ni namna ya kukabiliana na maisha kiuchumi. Jambo hili linatokana na ugumu wa kuajiriwa au kujiajiri. Kutokana na ugumu wa kuajiriwa, wahitimu wa ngazi mbalimbali kutafuta ajira hasa rasmi.

Kama mbadala wa kuajiriwa, baadhi hulazimika kujiajiri. Hata hivyo wapo wanaoamua kutoajiriwa badala yake kujiajiri hata kama wanapata kazi za kuajiriwa.

Pia wapo waliowahi kuajiriwa lakini wakaacha na kujiajiri au kuchanganya kuajiriwa na kujiajiri. Vijana wengi wanakumbana na changamoto kubwa katika azma ya kujiajiri. Kubwa ni upatikanaji wa mtaji.

Kwa nini vijana?

Kati ya maswali ya msingi kuhusu upatikanaji wa mtaji kwa wajasiriamali ni kwa nini kujikita katika kundi la vijana. Kundi hili ni kubwa sana nchini.

Kama ilivyo katika nchi nyingi zinazoendelea, Tanzania ni nchi yenye kundi kubwa la vijana ambao ni jeshi lenye nguvu, ubunifu na mtizamo chanya katika mambo kadhaa. Ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Kwa bahati mbaya kundi hili linakabiliwa na changamoto zaidi katika soko la ajira kuliko mengine. Hata kwenye mtaji, hali ni ngumu kwa vijana kuliko watu wazima.

Changamoto hizi zinasimama kati ya vijana wajasiriamali kwa upande mmoja na fursa kadhaa za ujasiriamali kwa upande mwingine.

Mahitaji ya mtaji

Wajasiriamali wengi wanahitaji mikopo kufanikisha malengo yao. Inaweza kuwa kuanzisha au kuendeleza biashara.

Katika hatua yoyote iliyofikia, biashara huhitaji fedha kugharamia shughuli mbalimbali. Mtaji unaweza kuhitajika kwa ajili ya kulipia pango la ofisi au eneo la kufanyia biashara, malighafi, wafanyakazi, usafiri, au vibali.

Kwa wajasiriamali wanaoanza, mtaji ni muhimu kufanikisha utekelezaji wa mawazo, mipango au njozi kuanzia hatua za mwanzo kwenda katika utekelezaji.

Kwa waliopo kwenye ujasiriamali, mtaji ni muhimu kuendeleza kilichopo na kukikuza katika hatua nyingine kubwa zaidi.

Changamoto kwa vijana

Japokuwa wajasiriamali wote hukabiliwa na changamoto ya mtaji, kundi la vijana lina changamoto za ziada.

Hizi ni changamoto zinazotokana na wao kuwa na umri mdogo wasio na uzoefu wa kutosha. Baadhi ya zinatoka upande wa ugavi wa uchumi kwa maana ya vyombo vya fedha na baadhi zinatoka upande wa uhitaji wa soko kwa maana ya vijana wenyewe.

Ni muhimu kuainisha na kuchambua changamoto hizi ili kupata suluhisho sahihi. Kati ya changamoto zinazotokana na taaisi za fedha zenye kutoa mikopo ni masharti ya mikopo husika.

Wakopeshaji

Ni muhimu kuelewa taasisi nyingi za fedha zipo kibiashara zaidi. Ni lazima zikidhi mahitaji ya msingi ya kibiashara na yale ya mamlaka dhibiti kama vile Benki Kuu ya Tanzania.

Hata hivyo ni ukweli kuwa masharti haya yanakuwa changamoto kwa wajasiriamali hasa vijana kwa ujumla na wale wanaotaka kuanza ujasiriamali kwa mara ya kwanza kimahususi.

Masharti haya ni pamoja na kuwa na leseni na vibali vya biashara, kuwa na ofisi maalumu na anwani ya mahali pa kufanyia biashahara au kuwa na biashara inayoendelea. Kwa hali hiyo, ni nadra kupata mkopo kwa ajili ya kuanzisha biashara. taasisi nyingi za fedha huepuka kukopesha wajasiriamali wa sekta ya kilimo kwa maana ya wakulima japo zipo tayari kukopesha kwa ajili ya biashara ya mazao.

Vijana wengi hawakidhi vigezo tajwa hapo juu. Hivyo ndoto za kujiajiri kama wajasiriamali zinakwamishwa na ukweli huo. Ndoto hizi zinapokwisha maana yake ni kuwa faida zinazotokana na ujasiriamali kama vile ajira, mapato ya Serikali, ukuaji uchumi na kupunguza umasikini nazo zinapotea.

Changamoto kwa vijana

Kimsingi, masharti yaliyotajwa hapo juu yanawahusu wakopaji wote bila kujali umri ingawa hangamoto zinakuwa kubwa na nzito zaidi kwa vijana kwa sababu ya hali zao.

Kwa vijana waliohitima ngazi mbalimbali za elimu, ni nadra kukidhi vigezo na masharti ya mikopo kutoka taasisi za fedha hasa benki za biashara zinazokusudia kupata faida.

Vijana wengi hawana mali zisizohamishika kama vile nyumba na ardhi. Na hawana hata hizo mali zinazohamishika kama magari. Kwa kijana anayetaka kuanza biashara kwa mara ya kwanza hatakuwa na taarifa za nyuma za biashara na hesabu zilizokaguliwa.

Vijana wengi hawana makazi wala anwani ya kudumu. Bado ni watafutaji na pengine wanapohitimu huondoka kwenda kutafuta maisha sehemu nyingine.

Hapa wanapoteza sifa ya kuwa na anwani maalumu kwa muda mrefu. Maana yake ni pamoja na kukosa mtandao na mtaji wa kijamii kama taasisi, marafiki na watu wanaoaminika, kufahamika na kuheshimika.

Mtandao na mtaji wa kijamii ni pamoja na Serikali za mitaa, viongozi wa dini na makundi kadhaa ya kiuchumi na kijamii.

Cha kufanya

Ni muhimu kila mdau atekeleze wajibu wake kurahisisha upatikanaji wa mitaji kwa vijana wajasiriamali. Taasisi za fedha lazima zifikiri tofauti na kuwaona vijana kama fursa badala ya kuonekana kama tishio kwao.

Ziwe na ubunifu na utayari wa kuwa na vigezo mbadala vya kutoa mikopo ikiwamo ya vitendea kazi vitakavyokuwa dhamana.

Vijana nao wajijengee na kujengewa uaminifu zaidi na taasisi hizi na jamii ili wakopesheke bila kujali ujana wao.

Serikali na wadau wengine wanaweza kuweka mazingira rafiki ili vijana wakopesheke kama vile kuwadhamini na kuwa na mtaji maalumu ya vijana.