Usipofungua kesi ndani ya miaka 12 utaipoteza ardhi yako

Thursday October 11 2018Justine Kaleb

Justine Kaleb 

By Jastine Kaleb

Haki ni anachostahili kupata mtu kwa mujibu wa sheria na wajibu ni anacholazimika kukifanya au majukumu ambayo mtu anapaswa kuyatimiza kwa mujibu wa sheria.

Kutimiza wajibu kutakupa nguvu na ujasiri wa kudai haki zako na kufahamu haki zako kutakuwezesha kumshurutisha mwingine atimize wajibu wake. Haki yako ni wajibu kwa upande mwingine na kinyume chake.

Kutojua haki zako kunakufanya uwe gizani na ushindwe kuona uhalisia wa unachostahili wala mwangaza wa wajibu wa mwingine kwako. Watu wanaangamia kwa kukosa maarifa.

Gharama ya kutojua haki zako kwa mujibu wa sheria za ardhi, ni kubwa sana kuliko gharama za kununua au kumiliki ardhi yenyewe.

Watu wengi wameonewa, kudhulumiwa hata kunyanyaswa katika ardhi zao wenyewe kwa sababu ya kutojua haki na wajibu wao. Hakuna kitu kibaya na cha kushangaza kama mwenyeji ukaonewa na kunyanyaswa na mgeni katika ardhi yako mwenyewe kwa sababu hujui haki zako kisheria.

Sheria za ardhi zinabainisha haki ulizo nazo. Ni wajibu wako kuzifahamu ili uzipate. Haki na wajibu wako kwa mujibu wa sheria zinaanzia katika Katiba ya nchi ya mwaka 1977.

Sheria za ardhi zinaeleza haki zako ni kumiliki ardhi bila kujali jinsia, kuuza, kununua, kutoa au kubadilisha umiliki baada ya kujiridhisha juu ya umiliki halali wa yule anayekuuzia.

Kupangisha au kukodisha ardhi yako kwa mtu mwingine, kuiendeleza kwa mujibu wa masharti na matumizi ya ya eneo husika, kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu yeyote ikiwamo na Serikali aliyevamia ardhi yako ni haki nyingine.

Vilevile, sheria inakuruhusu kuchukua hatua za kisheria dhidi ya mtu ambaye matumizi ya ardhi yake yanaleta madhara kwa wengine na kukata rufaa kutoka chombo kimoja cha sheria hadi kingine endapo utakuwa hujaridhika na uamuzi uliotolewa.

Unapaswa kulipwa fidia inayoendana na thamani ya ardhi pamoja na mazao au jengo lililopo katika ardhi endapo eneo lako litachukuliwa na Serikali kwa ajili wa matumizi ya umma au shughuli nyingine yoyote.

Sheria za ardhi pia zimeainisha wajibu wako ambao ni muhimu sana ukaufahamu ili uweze kuutimiza na kukupa uwezo wa kudai haki zako. Wajibu wako ni kuliendeleza na kulitunza eneo ulilopewa kisheria, kufanya matumizi sahihi na halali yaliyoidhinishwa katika masharti ya utoaji wa ardhi hiyo na kutobadilisha matumizi ya eneo ulilopewa pasipo idhini ya mamlaka husika.

Kufungua shauri la ardhi katika vyombo vya sheria ndani ya muda usiozidi miaka 12 baada ya mgogoro kutokea, ikizidi hapo utakuwa umepoteza haki yako.

Kutambua mahali kiwanja chako kilipo na chombo gani kina mamlaka ya kutatua migogoro ya ardhi katika eneo hilo na kujiridhisha juu ya haki na mamlaka ya umiliki wa yule anayekuuzia ardhi hiyo katika ofisi za ardhi au uongozi wa Serikali uliopo katika mtaa, kata, kijiji au wilaya husika.

Kulipa kodi za ardhi na majengo yaliyopo katika ardhi hiyo, kutofanya vitendo vyovyote vya uvunjifu wa sheria katika eneo unalolimiliki na kutouza eneo ulilopewa kisheria bila kuitaarifu mamlaka husika na kutoa taarifa unapoona kuna matumizi mabaya ya ardhi yanafanyika ni wajibu wako pia.

Fahamu haki zako na utimiza wajibu wako. Usikubali kuonewa au kudhulumiwa wakati sheria imetungwa kulinda haki zako. Chukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria na usiruhusu ardhi yako ipotee au mgogoro wowote utakaokupotezea muda wa kuitumia kwa faida unazozitaka.

Advertisement