Vijana nchini wanahitaji kambi za ujasiriamali

Thursday May 30 2019

Vijana wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheri

Vijana wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania(KKKT),Dayosisi ya Kaskazini wakiwa katika  Wiki ya Askofu na Vijana iliyofanyika wilayani Karatu mkoa wa Arusha jana. Picha na Filbert Rweyemamu 

By Honest Ngowi

Hakuna anayeweza kupinga umuhimu wa ujasiriamali nchini kwa sasa. Zipo juhudi zinazolenga kuendeleza ujasiriamali ikiwamo kupitia makongamano, warsha, mafunzo maalumu na kambi za ujasiriamali.

Kati ya kambi za ujasiriamali zinazofahamika zaidi kwa miaka ya karibuni ni inayofanywa na Chuo Kikuu cha Mzumbe. Kama zilivyo nyingine, kambi hii ni muhimu kwa vijana. Mwishoni mwa mwezi huu, itafanyika kwa siku mbili katika kampasi kuu iliyopo Morogoro.

Kwa mtazamo wa kiuchumi, ujasiriamali ni sehemu ya uzalishajimali kama ilivyo kwa ardhi, nguvukazi na mtaji. Mjasiriamali ndiye anayekusanya kila kinachohitajika ili kuanzisha uzalishaji na usambazaji wa bidhaa au huduma. Mjasiriamali hujiajiri na kuajiri wengine.

Mwaka 2019, Mzumbe inafanya kambi hii kwa mwaka wa tatu ambayo hujumuisha mawasilisho ya kitaaluma, uzinduzi wa kampuni za wanafunzi, bidhaa na huduma za wajasiriamali, maonyesho ya bidhaa na huduma, ushindani wa mawazo ya biashara na ushuhuda kutoka kwa waliofanikiwa.

Vijana ni nguvukazi muhimu na kubwa yenye nguvu, ubunifu, maono, njozi na uthubutu. Vyote hivi ni muhimu katika ujasiriamali. Kwa miaka ya karibuni, umuhimu na mvuto wa ujasiriamali kwa vijana umeongezeka kutokana na mabadiliko ya kisera na kifikra.

Sekta binafsi na uchumi wa soko vimepewa nafasi kubwa. Umuhimu wa kujiajiri badala ya kutegemea kuajiriwa umeongezeka kwa sababu ya mahitaji ya soko la ajira ambalo ni finyu lisiloweza kuchukua wahitimu wote.

Advertisement

Yanayotokea katika kambi za ujasiriamali ni muhimu katika kujenga ujasiri na kuchochea mafanikio kwa vijana.

Kambi za ujasiriamali kama zinazoendeshwa na Chuo Kikuu cha Mzumbe hufundisha kwa vitendo masuala muhimu yanayomuhusu mjasiriamali. Haya hufanywa na wataalamu na wazoefu wanaouishi ujasiriamali. Kambi hizi huonyesha kwa vitendo jinsi ujasiriamlai unavyohusu kutafuta na kuona fursa wengine wasipoziona.

Ujasiriamali unaweza kufanywa na yeyote, popote na wakati wowote. Maendeleo ya teknolojia hasa ya mawasiliano yamerahisisha zaidi hili.

Uzoefu wa kambi za ujasiriamali unaonyesha ili kufanikiwa, ni lazima mjasiriamali awe na uthubutu, ubunifu, kujituma, kujinyima na kuwa tofauti sokoni. Vilevile anapaswa kuwa mshindani, mwenye uamuzi sahihi na mvumilivu kwa sababu ujasiriamali sio lelemama.

Ni muhimu kupangilia mambo badala ya kukurupuka. Mpango wa biashara unaoonyesha njia itakayofuatwa na mjasiriamali ili afikie malengo yake nayo ni muhimu.

Mambo ya kuzingatia

Kambi za ujasiriamali zinasaidia kuwajenga vijana katika kufikiria na kuzingatia mambo ya msingi kabla ya kuwekeza. Vijana hufundishwa kufanya upembuzi yakinifu na utafiti wa kina kabla ya kuwekeza. Hii husaidia kupata masoko ya uhakika kwa bidhaa au huduma inayokusudiwa kuzalishwa.

Ni muhimu kuuliza na kupata majibu ya maswali ya msingi kama vile uwapo wa soko na ukubwa wake, namna ya kuingia katika soko hilo, ushindani uliopo na mambo mambo mengine ya msingi.

Kambi huwasaida washiriki kufikiria kuwashinda washindani wake iwe katika bei, ubora wa bidhaa au huduma, uzoefu, huduma kwa mteja au matumizi ya teknolojia.

Kambi za ujasiriamali huwawezesha washiriki kujifunza namna ya kuwekeza iwe ni kwa muda mfupi, wa kati na muda mrefu na sababu zake.

Husaidia washiriki kujua kama wanapaswa kuwekeza ili kupata fedha ndogondogo za kumudu maisha ya kila siku au kwa ajili ya kipato kikubwa cha mbeleni.

Humuonyesha mjasiriamali kuwa hapaswi kufuata mkumbo bali ajiridhishe kabla ya kuwekeza. Ni lazima kufikiria kabla ya uamuzi wa mwisho ili uwekezaji ufanywe kwenye eneo lenye faida kubwa zaidi. Ni muhimu kwa mjasiriamali kuanza mapema iwezekanavyo.

Hata hivyo uwekezaji hauna umri wa kuanzia wala ukomo. Kambi huonyesha ni muhimu kuwekeza katika biashara unayoifahamu vizuri na kama huifahamu basi jifunze kabla ya kuwekeza. Pia ni muhimu kuwekeza katika biashara unayoipenda na unayoweza kusimamia kiurahisi.

Kambi za ujasiriamali huonyesha maeneo ya kuwekeza na kanuni za kuzingatia. Eneo la kuwekeza hutegemea sana hali halisi kwa wakati na mahali husika .

Hutegemea fursa zilizopo na uwezo wa kuzitendea haki.

Ni muhimu kuwekeza katika biashara itakayokulipa, unayoimudu kimtaji, kiutaalamu, kiusimamizi na ambayo haitakutesa. Hizi ni baadhi tuu ya faida na umuhimu wa kambi za ujasiriamali.

Advertisement