Volt kuwa kampuni ya kwanza ya madini kupata mtaji DSE

Dar es Salaam. Baada ya kuwalipa wananchi fidia ya maeneo yao, Volt Resources inakamilisha utaratibu wa kuuza dhamana yake katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) na Mauritius (SEM) ili kupata mtaji utakaowezesha kukamilishwa kwa awamu ya kwanza ya uchimbaji wa madini grafiti Bunyu.

Mapema Januari, wananchi 776 kati ya 785 wa vijiji saba vya Kata ya Matambale wilayani Ruangwa, Lindi walilipwa Sh7.45 bilioni kufidia mazao yao ili kupisha mradi wa uchimbaji madini hayo.

Kwa sasa, Volt Resources inakamilisha waraka wa matarajio kuiwezesha kuuza dhamana (note) ili kupata Dola 40 milioni za Marekani zinazohitajika kama mtaji.

Ofisa mtendaji mkuu wa Volt Resources, Trevor Matthews kuorodheshwa kwa Amana hiyo kutasaidia kupata fedha zinazohitajika kukamilisha mradi huo na kuanza uchimbaji.

“Mckato unaendelea vizuri, kote, Tanzania na Mauritius. Mchakato wa Tanzania umechukua muda mrefu kuliko ilivyotarajiwa kwa sababu Volt ni kampuni ya kwanza ya madini kulitumia DSE kupata mtaji, ila tunakaribia kuhitimisha utaratibu uliopo,” amesema Matthews.

Ofisa huyo amesema mazungumzo yanaendelea vizuri baina yake na Serikali pamoja na mamlaka za mitaji na masoko kufanikisha upatikanaji wa mtaji huo kutokana na mikutano kadhaa iliyofanyika.

Msemaji wa Mamlaka ya Masoko na Mitaji (CMSA), Charles Shirima amethibitisha kuwapo kwa mchakato huo bila kutaja utakamilika lini.

“Kila hatua wanayofika wanaelekezwa taarifa zinazohitajika hivyo kasi yao ya kukamilissha ndio itakayoamua,” amesema Shirima.

Kuhusu dhamahana hiyo kuorodheshwa kwenye zaidi ya soko moja la hisa, amesema inawezekana na inategemea ukubwa wa fedha anazozihitaji mteja. “Endapo haziwezi kupatikana kwenye soko moja, kampuni inaweza kuuza dhamana yake kwenye masoko mawili,” amefafanua.

Volt ni kampuni ya pili kutangaza kuanza mchakato wa kutafuta mtaji wa kuchiba madini hayo. Aprili, kampuni ya Kibaran Resources ilisaini mkataba wa mkopo wa Dola 40 milioni na Benki ya KfW IPEX ya Ujerumani ili kukamilisha mradi wake uliopo Kijiji cha Epanko kilichopo Mahenge mkoani Morogoro.