Wachoraji, wachongaji wahudhuria maonyesho ya sanaa China

Dar es Salaam. Watanzania sita wawalikuwa kati ya maelfu ya walioshiriki maonyesho ya sanaa ya kimataifa nchini China.

Balozi wa Tanzania nchini China, Mbelwa Kairuki amesema kwa kuwa ni mara ya kwanza kwa wasanii wa Tanzania kushiriki maonesho hayo, ana imani mrejesho utakaotokana nao utahamasisha wengine kushiriki maonesho yajayo.

Kwenye maonyesho hayo, Tanzania ilipewa nafasi 20 lakini ushiriki umekuwa mdogo, huenda wasanii wengi zaidi hawakujitokeza kushiriki ili kuepuka gharama ya kusafiri bila kujua kama watapata masoko ya bidhaa walizonazo.

“Soko la Hong Kong ni zuri sana. Wasanii wetu walikuwa wanataka kuuza bidhaa zao kwa kati ya Sh200,000 hadi Sh1 milioni lakini wakaona wa mataifa mengine wanauza picha zenye ubora sawa na zetu kuanzia Sh10 milioni na kuendelea hivyo wakabadilika,” amesema Kairuki.

Kutokana na washiriki wa mwaka huu kuuza picha zao kwa bei nzuri, itawaongezea ari wao na kuwahamasisha wengine na idadi ya washiriki itakuwa kubwa zaidi kwenye maonyesho yajayo chini ya uratibu wa Baraza la Sanaa Tanzania.

Maandalizi ya maonyesho hayo yalianza tangu Januari na katibu mtendaji Godfrey Mngereza amesema ingawa Balozi Kairuki amefanya kazi kubwa, mwitikio wa wasanii haukuwa mkubwa kama ulivyotarajiwa.

“Mwanzo wasanii 13 waliahidi kushiriki lakini baadaye wakapungu ampaka 10 na mpaka mwisho walioenda ni hao sita pekee. Kuna changamoto ambazo baraza imejipanga kuzishughulikia ili kuongeza ushiriki wa Watanzania,” amesema Mngereza.

Amezitaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni woga wa wachoraji na wachongaji kujitokeza kwenye masoko ya kimataifa hata kupuituia mitandao ya kijamii. Wengi waliowafuata, amesema wamekuta hawana hata akaunti Facebook, Instagram au Tweeter maeneo ambayo ni rahisi kukutana na watu wa kimataifa.

Hata wachache waliopatikana, amesema hawana vipeperushi vinavyoelezea bidhaa zao wala taarifa fupi ya kampuni zao.

“Balozi alijitahidi kulipia gharama za maonyesho, kiasi cha Dola 15,000. Mwanzo ilikuwa walipie mabanda lakini wachache wakawa wanategemea kufadhiliwa gharama ningine,” amesema.

Ili kuwaongezea utambulisho wa kimataifa, amesema Basta imeanda mpango wa mafunzo kwa wasanii hao.