‘Wafugaji fuateni ushauri’

Muktasari:

Ofisa Masoko wa Shirika la BRAC kupitia mradi wa LEAD, Stephano Mahenge alisema hayo wakati akizungumza na wafugaji wa kuku na walaji.

Iringa. Wafugaji wa kuku nchini wametakiwa wafuate ushauri wa kitaalamu ikiwamo kuipima mifugo yao maabara kabla ya kununua dawa na kuwatibu.

Ofisa Masoko wa Shirika la BRAC kupitia mradi wa LEAD, Stephano Mahenge alisema hayo wakati akizungumza na wafugaji wa kuku na walaji.

Mahenge alisema tathimini waliyofanya kati ya Mei na Julai mwaka huu kwenye soko la Iringa wamebaini kuwa wafugaji wamekuwa wakinunua dawa za kutibu kuku wao bila ya kupata ushauri wa kitaalamu.

Hata hivyo, alisema wauzaji wa dawa wanatakiwa kuwadodosa wafugaji kabla ya kuwauzia dawa ili wapate uhakika wa magonjwa ya mifugo.

“Wafugaji huwa wanawaambia rafiki zao kuwa kuku wao walipokuwa wanasinzia walitumia dawa fulani, nao bila kupata maelekezo ya wataalamu wa mifugo wananunua dawa hizo na kuwapa kuku,” alisema mfugaji Kwangu Kitinga.

Ofisa Kilimo na Mifugo wa Manispaa ya Iringa, Richard Nyegela alisema ni vema wafugaji wakajenga mazoea ya kutumia dawa za kutibu kuku baada ya kupata ushauri wa wataalamu.

Alisema kupima kuku maabara ili kujua tatizo ni gharama yake ni Sh1,000 kwa ikilinganishwa na hasara anayoweza kupata mfugaji kwa kupotelewa na kuku wengi kwa wakati mmoja.

“Mnatakiwa kujenga utamaduni wa kupeleka maabara kupima kuku ili kujua tatizo badala ya kukimbilia kwenye maduka kununua dawa na kuanza kutibu bila kujua kujua ugonjwa unaomsumbua kuku,” alisema.

Pia, aliwataka watotoleshaji wa vifaranga kuwa na mashamba yao badala ya kutegemea mayai kutoka kwa wafugaji. Mtotoleshaji, Josia Byampanju alisema kwa sasa ubora wa vifaranga unategemea matunzo na kumbukumbu za mfugaji kwa kuwa ndiye anayejua jinsi anavyowatunza kuku wake.

Alisema wadau wa sekta hiyo wakiwamo wafugaji, watotoleshaji, wauzaji wa dawa na walaji wa kuku wanatakiwa kuwa wakweli wanapofanya shughuli zao ili kuhakikisha wanazalisha bidhaa bora.