Wateja wengi Benki ya Wananchi Mbinga hawajarudishiwa fedha zao

Dar es Salaam. Wakati Rais John Magufuli akiagiza kutafutwa kwa watu waliochangia kufilisika kwa iliyokuwa Benki ya Wananchi Mbinga (MCB), mkurugenzi mtendaji wa Bodi ya Bima ya Amana (DIB), Richard Malisa amesema wateja wengi bado hawajaenda kuchukua fedha zao.

Rais Magufuli alitoa agizo hilo mapema wiki hii alipokuwa ziarani wilayani humo ikiwa ni miaka miwili baada ya kufutwa kwa leseni ya MCB.

“Waliohusika watafutwe mara moja na kuona jinsi hawa wachache walivyonufaika,” alisema Magufuli.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT), ilitangaza kuifuta leseni ya MCB Juni 2017 kutokana na kukosamtaji wa kutosha kujiendesha.

BoT ilisema MCB ilipata hasara ya zaidi ya Sh2.4 bilioni hivyo kushindwa kujiendesha na kulipa madeni kwa wakati yakiwamo madai ya wenye amana.

Kumbukumbu zinaonyesha MCB ilikuwa haifanyi vizuri. Mwaka 2013 ilitangaza hasara ya ya Sh52.84 milioni ambayo iliyoongezeka mpaka Sh1.14 bilioni Desemba 2014 kisha Sh812.58 milioni mwaka uliofuata na Sh408.06 milioni mwaka 2016.

Mpaka Machi 31, 2017 mtaji wake ulishuka hadi hasi Sh2.88 bilioni hivyo kuishawishi BoT kuifunga.

Aliyekuwa mkurugenzi wa usimamizi wa benki na taasisi za fedha wa BoT, Kennedy Nyoni aliwahi kusema mapungufu ya uongozi na uendeshaji vilichangia MCB kushindwa kujiinua kutoka katika matatizo hayo.

“Uongozi ulishindwa kuhimili ushindani wa soko hivyo kupoteza biashara kwa washindani na kuendelea kupata hasara,” alisema Nyoni.

Baada ya kukamilisha taratibu zote za ufilisi, Julai 24, 2017 DIB ilitangaza kuanza kuwalipa wateja 13,000 wa MCB ambayo iliwahi kuhudumia zaidi ya wateja 26,000 enzi zake.

Benki hiyo ilikuwa na wateja 26,000 wakati inaanguka hivyo kupoteza mtaji wa wanahisa wake wakubwa ambao ni halmashauri za Mbinga Mjini na Vijijini, kiwanda cha kukoboa Kahawa Mbinga na Halmashauri ya Wilaya ya Nyasa.

Hata hivyo, mkurugenzi mtendaji wa DIB, Malisa anasema bado malipo hayo hayajakamilika. “Malipo yanaendelea kutolewa kwenye matawi ya Benki ya Posta. Tumeweka matangazo Mbinga na kila mteja anatakiwa kwenda huko kuchukua fedha zao. Bado wateja wengi hawajalipwa,” anasema.

Kutokuwapo kwa mawasiliano ya wateja waliotunza zaidi ya Sh1.5 milioni, anasema ni miongoni mwa changamoto zinazosababisha kukawia kwa.

“Ingewezekana kuwatumia wateja wote kwa M-Pesa au Tigo Pesa lakini hawakuwa wakiandika namba ya simu hivyo ni lazima waje benki kuchukua fedha zao,” anasema.