10 kortini kwa wizi wa Sh59.9 milioni za CRDB

Muktasari:

Washtakiwa wamefikishwa Mahakama ya Kisutu leo wakidaiwa kutenda kosa hilo Aprili 25 mwaka huu.

Dar es Salaam. Watu 10 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kujibu mashtaka manne ikiwemo wizi wa Sh59.9 milioni mali ya Benki ya CRDB.

Washitakiwa hao ni Abdul Mahamud, Hassan Kimangale, Deogratius Mtwale, Salim Mtandika, Geofrey Michael,  Wilberth Mwasongwe, Eliuphoo Swai, Arnold Natai, Rehema Alphany na Johnson Muyanda.

Akiwasomea hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Agustine Mbando, wakili wa Serikali Faraji Nguka amedai leo Mei 17, 2019 kuwa washitakiwa hao walitenda kosa hilo Aprili 25 mwaka huu jijini Dar es Salaam.

Amedai kuwa katika tarehe hiyo, washitakiwa Mahamud, Kimangale, Mtwale na Mtandika walikula njama ya kutenda kosa la wizi.

Katika shtaka la pili inadaiwa kwamba washtakiwa Mahamud, Kimangale, Mtwale, Mtandika, Michael, Ntai, Rehema na Mayunda, Aprili 25 mwaka huu eneo la Tazara Oilcom katika ATM ya CRDB waliiba Sh. 39,940,000 mali ya benki hiyo.

Katika shitaka lingine, washitakiwa hao kwa pamoja  wanadaiwa kuiba Sh20 milioni mali ya benki hiyo.

Katika la nne washitakiwa Mwasongwe na Swai, wanadaiwa kushindwa kuzuia wizi wa fedha hizo mali ya Benki ya CRDB.

Akitoa masharti ya dhamana Hakimu Mmbando alimtaka kila mshtakiwa kuwa  na wadhamini wawili kila mmoja atakaesaini bondi ya Sh3 milioni.

Wakili Nguka alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na imeahirishwa hadi Mei 31 mwaka huu na washitakiwa wote wamepelekwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.