UCHUMI: Mapato ya mrahaba wa madini yashuka

Sh130 bil:Mapato ya madini mwaka 2013/2014
Sh146 bil: Mapato ya madini mwaka 2012/2013

Muktasari:

  • Dhahabu katika soko la dunia nayo inazidi kuporomoka

Dar es Salaam. Mapato ya Serikali yatokanayo na mrahaba katika sekta ya madini kwa kipindi cha miaka miwili yameshuka kwa takribani Sh16.2 bilioni.

Kwa mujibu wa ripoti mbili mpya za mpango wa kuhamasisha uwazi na uwajibikaji katika sekta ya madini, mafuta na gesi (Teiti), mwaka wa fedha wa 2013/2014 mapato yalikuwa Sh130.6 bilioni ikilinganishwa na Sh146.8 bilioni ya mwaka 2012/2013.

Katika mwenendo huo, ripoti ya mwaka 2012/2013 inaonyesha wizara hiyo ilipata Sh132.9 bilioni ikiwa ni mrahaba, Sh13.6 bilioni kwa ajili ya ada na leseni za ukodishaji rasilimali na Sh305.8 milioni kwa ajili ya gharama nyinginezo.

Hata hivyo, ripoti hizo zinaonyesha hali haikuwa nzuri kwa mwaka wa fedha 2013/2014 ambao wizara hiyo ilipata Sh116.8 bilioni ikiwa ni mapato ya mrahaba na Sh13.7 bilioni katika tozo na leseni.

Watalaamu wa masuala ya madini wanahusisha kushuka huko kwa mapato kwa asilimia 11 na kuporomoka kwa bei ya dhahabu katika soko la dunia na kupungua uzalishaji madini nchini.

“Hali hii inaweza kuelezewa kwa kushuka kwa uzalishaji wa madini nchini hasa baada ya kufungwa kwa migodi ya Golden Pride wa Nzega na Tulawaka wilayani Biharamulo ambao hata baada ya (Kampuni ya Madini ya Serikali) Stamico kuuendeleza bado uzalishaji hauridhishi,” alisema Mkurugenzi wa Ukaguzi na Uzalishaji na Biashara ya Madini kutoka Wakala wa Usimamizi na Ukaguzi wa Madini (TMAA), Liberatus Chizuzu,

Alisema bei ya dhahabu katika soko la dunia nayo inazidi kuporomoka kiasi cha kupunguza mapato kwa Serikali kwa kuwa sasa wakili moja inauzwa kwa wastani wa Dola 1,100 za Marekani kutoka Dola 1,800.