SBL yakoleza kampeni ya unywaji kistaarabu Moro

Mkuu wa  Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Morogoro (RTO), Michael Deleli akimkabidhi kifaa cha usalama barabarani (Reflectors) Yusuph Ramdhan ambaye ni dereva bodaboda mkoani humo wakati wa uzinduzi wa Kampeni ya Unywaji kiistaarabu ijulikanayo kama “Usinywe na Kuendesha” inayoratibiwa na Kampuni ya bia ya Serengeti Breweries (SBL).

Dar es Salaam. Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) imeendelea na kampeni yake ya uelimishaji juu ya unywaji kiistarabu inayolenga kuwafikia wanafunzi wa vyuo, madereva, waendesha vyombo vya umma na madereva bodaboda mkoani Morogoro.

Kampeni hiyo ya siku mbili ijulikanayo kama 'Usinywe na Kuendesha Chombo cha Moto' ilifanyika mwishoni mwa wiki iliyopita na imelenga kuwafikia watu 1,000 kupitia maeneo mbalimbali ikiwamo sehemu za starehe ‘baa’, vyuo pamoja na watumiaji wengine wa barabara.

Kampeni hiyo ilizinduliwa wiki iliyopita katika Hoteli ya Nashera ambapo wadau mbalimbali wa usafirishaji ikiwamo Jeshi la Polisi, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra) na madereva walishiriki.

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugeni wa Uhusiano wa SBL, John Wanyancha kampeni hiyo imelenga kuwafikia watu 1,000 wakazi wa Mkoa huo ikiwa ni mkakati wa kuunga mkono jitihada za Serikali katika kupunguza kiwango cha ajali za barabarani hapa nchini.

Mkurugenzi huyo alisema kampuni hiyo inashirikiana na wadau mbalimbali ikiwamo Jeshi la Polisi-Kitengo cha Usalama Barabarani ambapo kampeni hiyo imeshafanyika katika mikoa ya Mwanza na Dar es Salaam mwanzoni mwa mwaka huu.

“Katika kampeni hii tunatoa vifaa mbalimbali vya uelimishaji ikiwamo vipeperushi, vibandiko (stika), makoti ya usalama (reflectors), fulana pamoja na kuwashirikisha wadau katika majadiliano yanayolenga katika kutokomeza baadhi ya mila na desturi potofu juu ya matumizi ya pombe,” alisema Wanyancha.

Aliongeza, “Unywaji kistaarabu hauishii tu katika kupunguza kiwango cha pombe bali ni kutokuruhusu pombe itawale maisha yako au iongoze mahusiano yako.”

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Morogoro (RTO) Michael Deleli aliishukuru SBL kwa jitihada hizo na kwamba kwa kulishirika Jeshi la Polisi ni chachu ya kuleta mabadiliko chanya na kuzifanya barabara kuwa salama  kwa watumiaji.

Hatahivyo, Deleli alisema anasikitishwa na vitendo vya baadhi ya madereva kunywa pombe kiholela pasipo kujali matokeo yake huku akitoa wito kuwa tabia hizo zinatakwa kukoma ili kupunguza ajali zinazowza kuepukika.

“Jeshi la Polisi, madereva, watembea kwa miguu na makampui kama hii ya Serengeti na jamii kwa ujumla tuna wajibu wakuhakikisha kuwa barabara zetu zinakuwa salama kwa kuhamasisha madereva kuzingatia unywaji kiistarabu,” alisema Deleli.

Aliongeza, “Nafarijika kuona kwamba licha kuwa ni Serengeti ni wazalishaji wa bia lakini wamejitoa kwa ajili ya kupambana na tatizo la ulevi hasa kwa maadereva ambao wanabeba dhamana ya maisha ya watu wengi,” alisema Deleli.