Airtel yapunguza bei ya huduma za simu

Muktasari:

  • Mtandao wa simu wa tatu kwa ukubwa nchini (Airtel) umetangaza kupunguza gharama za bei za huduma zake za simu, ujumbe mfupi na internet kwa asilimi 80. Mtandao huo unawateja takribani milioni 11.

Dar es es Salaam. Kampuni ya simu ya Airtel imepunguza gharama za huduma zake kwa wastani wa asilimia 80 kutokana na kile kilichoelezwa kuwa ni kuendana na mahitaji ya wateja na kuongeza uhuru wa kuongea.

Hatua hiyo imetangazwa leo Mei 22, 2019 wakati wa mkutano wa kampuni hiyo na waandishi wa habari uliofanyika jijini hapa.

Mkurugenzi wa masoko wa Airtel, Isack Nchunda alisema sasa watumiaji wa Airtel wataweza kupiga simu ndani na nje ya mtandao kwa Sh1 tu kwa sekunde tofauti na awali ambapo gharama ilikuwa Sh5 kwa sekunde ndani ya airtel na Sh7.6 kwenda mtandao mwingine.

"Kabla ya kuanzishwa huduma hii ambayo haihitaji kujiunga, Sh500 ulikuwa unaweza kupiga simu kwa dakika moja na nusu lakini sasa itakuwa dakika nane, pia Mb moja sasa itapatika kwa Sh40 tofauti na awali ambapo ilikuwa Sh172 huku bei ya ujumbe mfupi ikipungua kutoka Sh50 hadi Sh10, " amesema Nchunda.

Amesema hii ni huduma mpya ya Airtel na si promosheni hivyo haina muda wa ukomo na imekuja kutokana na malalamiko ya wateja ambayo wamekuwa wakiyatoa mara kwa mara ingawa vifurushi vya mtandao huo vitaendelea kuwepo kama kawaida.

Mkurugenzi wa mawasiliano wa Kampuni hiyo Beatrice Singano amesema huduma hii inawafurahisha zaidi watu wasiopendelea kujiunga bando na kwa kupunguza gharama hizo anaamini wataongeza idadi kubwa ya wateja.

"Umefanyika utafiti wa kibiashara kabla ya kuja na huduma hii, hatutarajii athari za kupungua kwa mapato lakini tunatarajia kuongeza mapato na  idadi ya wateja (bila kutaja ni kwa asilimia ngapi)," amesema Singano.