Benki tano zapigwa faini ya Sh1.8 bilioni na BoT

Muktasari:

  • Taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ya Septemba 19, 2019 imesema benki tano zimepigwa faini baada ya kubainika kukiuka kanuni za sheria inayozizuia kutakatisha fedha.

Dar es Salaam. Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imezipiga faini ya Sh1.88 bilioni kwa benki tano nchini humo kutokana na kukiuka kanuni namba 17, 20 na 28 za sheria inayozuia utakatishaji wa fedha haramu ya mwaka 2012.

Benki zilizopigwa faini hiyo ni benki ya African Banking Corporation Sh145 milioni, Equity Bank (Tanzania) Sh580 milioni, Benki ya I&M Bank (Tanzania) Sh655 milioni, Benki ya UBL Tanzania Sh325 milioni na Benki ya Habib African Sh175 milioni.

BoT imesema benki hizo zilishindwa kuhakiki taarifa za utambulisho wa wateja na kushindwa kuwasilisha taarifa ya miamala yenye kuleta mashaka katika Kitengo cha Kuzuia Fedha Haramu (FIU).

Taarifa iliyotolewa na BoT Septemba 19, 2019 ilieleza mbali na faini hiyo benki hizo zitapaswa kuhakikisha zinarekebisha kasoro zilizobainika ndani ya kipindi cha miezi mitatu tangu kutolewa kwa adhabu hiyo.

Benki hizo zimetakiwa kupitia upya taarifa za wateja wao na kuhakikisha kwamba zinakidhi matakwa ya kisheria na kanuni zilizopo za uhakiki wa utambulisho wa wateja (KYC) na Kuwasilisha taarifa ya miamala yenye kuleta mashaka ambayo ilitakiwa kuwasilishwa FIU.

Pia kufanya tathmini ya ubora wa mifumo ya ndani ya kibenki na kuchukua hatua stahiki kuhakikisha mifumo hiyo ipo madhubuti kwa lengo la kukinga mapungufu hayo hayarudii tena na Kuwachukulia hatua stahili wafanyakazi wote waliohusika kufanikisha ufunguaji wa akaunti za amana kinyume na kanuni za kumtambua mteja (KYC).