Benki ya NBC yatanua huduma zake kupitia Shirika la Posta

Muktasari:

Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na Shirika la Posta Tanzania wameingia makubaliano ya kusogeza huduma za kifedha kwa wananchi hasa maeneo ya vijijini.

Dar es Salaam.  Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imeingia makubaliano ya uwakala wa huduma za kibenki na Shirika la Posta Tanzania ili kupanua wigo sambamba na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha hasa maeneo ya vijijini.

Hatua hiyo inatajwa kuwa itaongeza wigo wa mtandao wa utoaji huduma za kifedha kwa njia ya kidijitali huku ikienda sambamba na azma ya serikali ya kupanua ushiriki wa wananchi katika shughuli za kifedha (financial inclusion).

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini mkataba wa kutoa huduma za kibenki kati ya Posta na NBC jijini Dar es Salaam leo Jumatano Septemba 18,2019, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema kupitia mtandao wa ofisi za Shirika la Posta lenye matawi 370,  kutaiwezesha NBC kuwafikia maelfu ya wananchi nchi nzima katika utoaji wa huduma zake kwa gharama nafuu.

“Ushirikiano huu kati ya NBC na Posta utawezesha ukusanyaji wa kodi na maduhuli ya Serikali kwa urahisi zaidi. Kwani ulipaji wa kodi na ukusanyaji wa maduhuli ya serikali yatafanyika katika mazingira salama na rafiki kwa wananchi kupitia ofisi za Posta, ”amesema Kamwelwe.

Amesema wafaidikaji wa ushirikiano huu kati ya NBC na Posta sio tu wateja bali watakuwepo wastaafu, wanafunzi, wakulima, wazazi na wafanyabiashara,’’amesema

Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi amesema ushirikiano huo utawawezesha kutumia mifumo ya kidijitali na wingi wa ofisi za posta katika kutoa huduma za kibenki nchi nzima.

“Kwa sasa NBC ina mawakala wapatao 2,000 na hivyo kuungana na Shirika la Posta, kupitia mtandao wa ofisi zake 370, kutatuwezesha kuongeza idadi ya wananchi watakaofikiwa na huduma za kibenki kwa ukaribu,’’ amesema

Amesema ushirikiano huo ni utekelezaji wa maelekezo ya serikali kwa mabenki ya kupeleka huduma ya kifedha kwa wananchi hasa walioko mikoani na vijijini.

Kwa upande wake, Posta Masta Mkuu, Hassan Mwang'ombe amesema kwa kuanza shirika hilo na NBC wataanza kutoa huduma katika ofisi 99 zilizo maeneo mbalimbali nchini.

“Huduma hizi ni zile zote za kibenki, kukusanya mapato ya serikali, kuhamisha na kutuma fedha, kufungua akaunti pamoja na huduma nyingine za kibenki.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Posta, Luteni Kanali mstaafu Dk  Haroun Kondo amesema kulingana na mageuzi ya kimfumo na maboresho mbalimbali yanayofanywa sasa na shirika hilo, yatatoa nafasi bora kwa taasisi na kampuni mbalimbali kuvutiwa kuweka ofisi au kuingia ubia wa kutoa huduma au uwakala wa huduma zake.