Bodi: Miwa ya wakulima Kilombero ilikosa ubora

Muktasari:

Bodi ya Sukari Tanzania imesema Kiwanda cha Sukari cha Kilombero cha mkoani Morogoro, kilitakaa kuchukua miwa kwa wakulima wanaokizunguka kutokana na kukosa ubora baada ya kukatwa na kuchomwa moto.

Dar es Salaam. Bodi ya Sukari Tanzania imesema Kiwanda cha Sukari cha Kilombero cha mkoani Morogoro, kilitakaa kuchukua miwa kwa wakulima wanaokizunguka kutokana na kukosa ubora baada ya kukatwa na kuchomwa moto.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi hiyo, Henry Semwanza, wakati akitoa taarifa ya uchunguzi wa malalamiko ya wakulima hao kwa vyombo vya habari jana baada ya miwa hayo kukataliwa na kiwanda hicho hivi karibuni.

Semwanza alisema kuwa baada ya uchunguzi kufanyika na kupokea malalamiko ya wakulima hao, wamebaini kuwa chanzo chake ni miwa hiyo kukosa sifa baada ya kukatwa, kuchomwa moto na kukaa kwa siku tano bila ya kuchukuliwa na kiwanda hicho kwa ajili ya kusindikwa na kutengeneza sukari.

“Miwa hiyo ilichomwa tangu Novemba 14, 2015, siku ambayo kiwanda kiliharibika na kilipotengamaa zilikuwa zimepita siku tisa, hivyo miwa kukosa sifa na ubora unaokubalika na kuzuiwa kuingia kiwandani.”

Uchunguzi huo ulifuatia agizo la Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Sophia Kaduma baada ya wakulima hao kukilalamikia kiwanda hicho kwa kukataa kununua miwa yao na kupata hasara ya Sh16 milioni.

Akizungumzia utekelezaji wa mkataba wa ugavi wa miwa baina ya kampuni na vyama vya wakulima, Semwanza alisema unasisitiza kutokubali miwa ambayo kiwango chake cha ubora kiko chini ya asilimia 80 au miwa iliyopitisha siku tano tangu ilipochomwa. Ili kupunguza hasara inayoweza kutokea kwa wakulima, Semwanza aliwakumbusha wakulima na wamiliki wa kiwanda hicho kuzingatia taratibu za uvunaji miwa.

“Ninatoa wito kwa wakulima kupitia vyama vyao kuzingatia taratibu za uvunaji kwa kuwa imedhihirika baadhi wamekuwa wanavuna miwa mingi zaidi ya mgao wao wa siku,” Semwanza.

Alisema bodi hiyo inaendelea kufuatilia utekelezaji wa makubaliano kati ya kiwanda na wakulima hao na kuonya kuwa haitasita kuchukua hatua kwa upande utakaokiuka ili kutatua migogoro inayoweza kuzuilika.

Semwanza alisema kwa sasa hali ni shwari na uvunaji na upokeaji wa miwa kiwandani hapo unaendelea na wakulima wameongezewa mgawo wa miwa inayotakiwa kuingizwa kila siku. “Mgao wa wakulima kuingiza miwa yao kiwandani umeongezwa kwa zaidi ya asilimia 50 ili kuhakikisha miwa yote ya wakulima wanaozunguka kiwanda cha Kilombero inavunwa, ” alisema.