CBA, Vodacom yawaongezea mzuka washindi ulipaji kodi

Wednesday December 19 2018

Mmoja wa washindi wa Bajaji., Mariam Barawa

Mmoja wa washindi wa Bajaji., Mariam Barawa akikabidhiwa zawadi yake na mwakilishi wa Mkurugenzi wa Benki ya CBA, Julius Konyani (kushoto) na mwakilishi wa Vodacom Tanzania, Noel Mazoya 

By Imani Makongoro, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Wakati Rais John Magufuli akisisitiza ulipaji kodi kwa wafanyabiashara nchini, washindi wa bajaji tano waliotokana na kampeni ya Benki ya CBA wamesema hawatafanya kosa kukwepa kodi watakapoanza kuzitumia kibiashara.

Washindi hao wa kampeni ya Shinda na M-Pawa inayoendeshwa na benki hiyo kwa kushirikiana na Vodacom, walisema hayo jana walipokabidhiwa bajaji hizo jijini Dar es Salaam.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, washindi hao walisema bajaji hizo zinakwenda kubadilisha uchumi wao kwa kuzitumia kujiongezea kipato huku wakizingatia ulipaji kodi.

“CBA na Vodacom wamenikwamua kwa kunipa bajaji nitaifanyia biashara lakini ili niwe salama kwanza ni kuzingatia kulipa kodi,” alisema Mariam Barawa wa Dar es Salaam.

Mshindi mwingine, Abeid Abdullah wa Chalinze mkoani Pwani, alisema ataendesha biashara ya bajaji kwa kufuata taratibu zote.

Akizungumza kwa niaba ya CBA, Julius Konyani alisema washindi hao ni kati ya wengine 1,296 wa kampeni hiyo iliyofanyika kwa wiki sita nchini waliopewa zawadi mbalimbali tofauti.

Naye mwakilishi wa Vodacom, Noel Mazoya alisema washindi hao wamepatikana kwa kuweka akiba kwenye M-Pawa sanjari na benki ya CBA, hivyo wanaamini wataendeleza tabia hiyo.

Advertisement