CEOrt kujadili fursa za kilimo nchini

Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt,  Santina Benson

Muktasari:

  • Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini(CEOrt) umeandaa warsha ya siku moja leo Jumanne Oktoba 16, 2018 utakayozikutanisha taasisi za utunzaji wa mazingira, kilimo na sekta ya fedha

Dar es Salaam.  Wadau wa kilimo nchini wanakutana kujadili fursa zilizopo katika sekta ya kilimo sanjari na kuzitafutia suluhisho changamoto zinazowakabili.

Umoja wa Maofisa Watendaji Wakuu wa Kampuni Binafsi nchini(CEOrt) umeandaa warsha ya siku moja leo Jumanne Oktoba 16, 2018 utakayozikutanisha taasisi za utunzaji wa mazingira, kilimo na sekta ya fedha.

Katika ufunguzi wa washa hiyo Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt,  Santina Benson amesema kilimo kimetoa ajira kwa watu wengi lakini kinashindwa kuwa chenye manufaa na endelevu kwa sababu wakulima wanakabiliwa na changamoto nyingi.

"Tumeona changamoto ndiyo maana tumeandaa washa hii ili tujadili kwa pamoja hapa kuna washauri wa kilimo wataeleza namna gani kilimo kinaweza kuboreshwa lakini pia kuna watu kutoka sekta ya fedha tutajadiliana nao kuhusu mitaji kwa wakulima," amesema Benson.

Amesema mabadiliko ya tabia ya nchi hapa nchi yanahatarisha uzalishaji ambao matokeo yake ni ukosefu wa chakula cha kutosha lakini pia kukwamisha maendeleo endelevu.

Kwa upande wake Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya kuendeleza kilimo kusini mwa Tanzania, Geoffrey Kirenga amesema kilimo cha kisasa kinachotegemea teknolojia kinahitaji kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi lakini changamoto ni wakulima kukifikia.

"Wakulima wanahitaji taarifa za kilimo, pembejeo na mitaji kwa ajili ya kilimo endelevu lakini yote haya hayajawezekana ndiyo maana uzalishaji sio wa kuliridhisha, fursa ni nyingi hususan katika kilimo biashara lakini changamoto zilizopo ni kikwazo," amesema Kirenga.