Faida ya Vodacom yapanda

Dar es Salaam. Licha ya misukosuko kadhaa iliyokabiliana nayo, mapato ya Vodacom yamevuka Sh1 trilioni kwa mwaka unaoishia Machi 31 na faida yake kabla ya kodi kuongezeka kwa asilimia 29.7.

Ndani ya kipindi hicho, taarifa za fedha za kampuni zinaonyesha ilipata Sh1.02 trilioni ikilinganishwa na Sh977.99 bilioni ilizopata mwaka ulioishia Machi 31, 2018.

Kutokana na mapato hayo, faida ya utendaji au faida kabla ya kodi ilifika Sh115.33 bilioni kutoka Sh88.9 bilioni iliyopata mwaka jana, lakini faida halisi ikashuka kutoka Sh170.24 bilioni iliyopatikana mwaka jana hadi Sh90.76 bilioni mwaka huu.

Faida halisi kubwa ya mwaka jana, taarifa zinaonyesha ilichangiwa na mauzo ya mali ya kudumu na si shughuli za biashara za kampuni hiyo. Itakumbukwa, mwaka jana kampuni hiyo iliiuza kampuni tanzu yake ya Helios Towers kwa Dola 58.5 milioni na kupata faida ya Sh120.25 bilioni.

Akibainisha sababu za ufanisi huo, mkurugenzi wa fedha wa Vodacom, Jacques Marais alisema ndani ya mwaka huo wamefanikiwa kuongeza wateja milioni 1.2 na kufikisha milioni 14.1. “Tutaendelea kuimarisha thamani ya hisa zetu na kuiongoza Tanzania kwenye safari ya kidigitali,” alisema.