Halotel yarejesha faida kwa jamii

Mkurugenzi wa kampuni ya Halotel, Nguyen Van Son(wa kwanza kushoto) akikabidhi hundi ya shilingi milioni 20.6 kwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Binilithi Mahenge (wa kwanza kulia) kwa ajili ya kuanzisha kiwanda cha kufyatua matofali cha kikundi cha vijana wa Dodoma, akishuhudia makabidhiano ni Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye (katikati)

Muktasari:

  • Katika mpango huo wa kurejesha faida kwa jamii, Halotel imetoa msaada utakaowawezesha vijana kujiajiri pamoja na misaada mingine katika Hospitali ya Makole.

KATIKA kuhakikisha inatekeleza agizo la Serikali kurejesha faida kwa jamii, kampuni ya simu ya Halotel imemkabidhi mkuu wa mkoa wa Dodoma zaidi ya Sh20 milioni kwa ajili ya kuwawezesha vijana wa mkoa huo kujiajiri kupitia sekta ya ujenzi.

Mbali na fedha hizo, Halotel pia imekabidhi vifaa mbalimbali vya hospitali kwa ajili ya kuhudumia wagonjwa vikiwemo vitanda, neti, mashuka na aproni vyenye thamani ya zaidi ya Sh6 milioni katika Hospitali ya Makole iliyopo Dodoma.

Akikabidhi misaada hiyo kwa mkuu wa mkoa wa Dodoma Dkt. Binilithi Mahenge mbele ya naibu waziri wa uchukuzi na mawasiliano Atashasta Nditiye, mkurugenzi mtendaji wa Halotel, Tanzania, Nguyen Van Son alisema pamoja na mambo mengine, misaada hiyo imelenga kuunga mkono juhudi mbalimbali za maendeleo zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano.

Son alisema, Halote, imekuwa mstari wa mbele kurudisha faida kwa kile inachokipata kwa kuisaidia jamii mambo mbalimbali  ili kukabiliana na changamoto zinazowazunguka.

Alisema hatua hiyo imelenga kutoa shukrani kwa wananchi kwa hatua yao ya kuwaunga mkono kwa kutumia huduma za kampuni hiyo iliyosambaa nchi nzima ikitoa huduma mbalimbali  na hasa maeneo ya vijijini.

“Tunaamini misaada hii itakwenda kuwa chachu ya maendeleo katika sekta ya afya na ujenzi, hususani kwa kuwawezesha vijana kujiajiri katika sekta za ujenzi unaoendana na kukua kwa mji wa Dodoma,” alisema Son.

Naye mkuu wa mkoa wa Dodoma Dk Binilithi Mahenge, pamoja na kuipongeza Halotel alisema msaada huo umekuja wakati muafaka kwani mkoa huo unaendelea na mikakati yake ya kuwasaidia vijana.

“Vijana wa Dodoma mtanufaika na Serikali kuhamia Dodoma, kupitia fedha hizi tumeona tuanzishe kikundi cha vijana ili waweze kuanzisha kiwanda cha kufyatua matofali na mradi huo utakuwa na vijana wa kutoka Jeshi la Kujenga Taifa ili wawasaidie ili baadae vijana waweze kuanzisha na kuendeleza viwanda vyao,” amesema Dkt. Mahenge.

Kwa upande wake mganga mfawidhi wa hospitali ya Makole Dk Geogre Matiko, aliishukuru Halotel kwa msaada huo huku akizitaka taasisi nyingine kuiga mfano huo.