Itachukua muda, fedha nyingi Dar es Salaam kuwa jiji la kisasa

Thursday March 28 2019Joyce Msuya aliteuliwa kuiongoza UNEP

Joyce Msuya aliteuliwa kuiongoza UNEP 

Baada ya kuitumikia Benki ya Dunia kwa zaidi ya miaka 20, Joyce Msuya ameteuliwa kuwa naibu mkurugenzi mtendaji wa Programu ya Mazingira ya Umoja wa Mataifa (UNEP) tangu Novemba mwaka jana.
Kwa wiki mbili mpaka Machi 15, Mtanzania huyo aliongoza mkutano wa nne wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa (Unea). Mwandishi wetu, Julius Mnganga alipata nafasi ya kuzungumza naye mambo kadhaa.
Swali: Mkutano wa nne wa Baraza la Mazingira la Umoja wa Mataifa ni nini na una maana gani kwa Watanzania?
Joyce: Mkutano wa baraza hili ni sehemu inayowakutanisha viongozi kutoka mataifa yaliyoendelea na yanayoendelea pamoja na wadau wengine kujadili changamoto za mazingira zilizopo na kuzitafutia suluhu ya kudumu.
Wadau hubainisha changamoto na kuweka mikakati ya kuzishughulikia. Huangalia mapungufu ya sera zilizopo na kuboresha. Ni sehemu ambayo sauti ya Tanzania inaweza kusikika kimataifa.
Watanzania wanaweza kuutumia kubadilishana mawazo na mataifa mengine. Hapa pia Tanzania inaweza kuuambia ulimwengu mafanikio iliyopata kwenye sekta ya mazingira.
Kama yalivyo mataifa mengine, Tanzania inayo nafasi ya kunufaika kwa kubadilishana uzoefu wa kushughulikia changamoto zilizopo nyumbani. Katika mkutano huu, kuna wadau kutoka sekta binafsi wakiwamo wanaharakati na kampuni pia.
Swali: Tanzania inatekeleza sera ya uchumi wa viwanda ambayo kwa namna moja inahusisha mazingira. Unadhani nini kizingatiwe kufanikisha nia hiyo?
Joyce: Changamoto zilizopo kwenye mazingira hazijali mipaka ya nchi. Changamoto zilizopo nchini zinahitaji sekta na wadau wote kuzishughulikia.
Serikali inapotekeleza sera ya viwanda ni vyema ikawashirikisha wawekezaji na wafanyabiashara kupanga namna viwanda vitakavyojengwa au maendeleo vitakayoleta yatakuwa sehemu ya kutatua badala ya kuwa chanzo cha tatizo.
Kama unavyoona katika mkutano huu, kuna wawakilishi wa Serikali, wafanyabiashara, vijana, wanaharakati na kampuni binafsi. Kila mmoja ana nafasi ya kukabiliana na changamoto za mazingira.
Swali: Ndani ya miaka mitatu ya Serikali ya Awamu ya Tano, kuna chochote kimekuvutia zaidi?
Joyce: Kama Mtanzania, sijaona tatizo kubwa. Nimeishi nchi nyingi duniani, Tanzania bado inafanya vizuri kimataifa.
Inapendeza kuiangalia Tanzania ukiilinganisha na mataifa mengine.
Leo nimekutana na mawaziri wa nchi nyingi wanaongelea ukame na wananchi wao wanakabiliwa na njaa. Wengine wanalalamika kukosa maji. Tanzania hatuna changamoto hizo, tunapoizungumzia nchi yetu ni vyema kuangalia wengine Afrika wakoje na changamoto walizonazo.
Swali: Athari za mabadiliko ya tabianchi na uchafuzi wa mazingira huchangia umasikini kwa kuwa hurudisha nyuma juhudi za wananchi. Unadhani Tanzania ifanye nini kutoka kwenye mtego huo?
Joyce: Ni kweli, athari nyingi za mazingira iwe uchafuzi wake au mabadiliko ya hali ya hewa, wanaoumia zaidi ni masikini kwa sababu uwezo wao wa kuzikabili ni mdogo.
Uzoefu kutoka nchi nyingi unaonyesha iwapo kutakuwa na nia ya dhati kutoka serikalini kwa mfano, kuzuia matumizi ya mifuko ya plastiki kama ilivyofanywa hapa Kenya, inawezekana. Mtazamo na utayari wa Serikali kutunga sera stahiki ni kitu muhimu.
Pili ni kuwasaidia masikini kupata mbadala wa suluhu zitakazopendekezwa. Zipo baadhi ya nchi hutoa ruzuku, nyingine hushirikiana na sekta binafsi kuwasaidia wasiojiweza.
Kwenye kilimo, mkulima mdogo wa kijijini apewe elimu. Unep tunafanya hivyo. Sisi tunashauri jinsi mkulima anavyoweza kuchagua mbegu nzuri zinazovumilia ukame na magonjwa, na madhara kidogo kwenye mazingira.
Nchini Tanzania tunao mradi wa kudhibiti taka kwenye miji tunaoshirikiana na UN Habitat.
Swali: Ingawa Dar es Salaam ni mji mkubwa, miundombinu yake ya ukusanyaji na uzoaji taka bado ni duni hivyo mvua ya muda mfupi tu husababisha mafuriko. Unashauri nini kuondokana na hali hii?
Joyce: Ukiangalia vipaumbele vya Serikali ni ujenzi wa miundombinu, upangaji wa miji pamoja na udhibiti taka. Rais mara zote anasisitiza hilo. Lakini tufahamu suala hilo linahitaji fedha nyingi na inachukua muda mwingi kulishughulikia.
Dar es Salaam ni mji wa zamani, kinachotakiwa ni kuufanya uendane na mahitaji yaliyopo ingawa hugharimu zaidi.
Niliwahi kuishi kwenye mji mmoja Korea Kusini ambao ulijengwa kwa mkakati maalumu, ilikuwa rahisi kwao kuupanga kama wanavyotaka.
Kazi bado ipo lakini kwa jinsi Serikali inavyojenga miundombinu naamini itawezekana, fursa zilizopo zitafunguka na Tanzania itaendelea.
Swali: Kuna matumizi yasiyo sawa ya rasilimali mfano maji, gesi au mafuta. Unapendekeza nini kifanyike kupata usawa?
Joyce: Hata kwenye nchi zilizoendelea, hali iko hivyo, si Tanzania pekee. Niliwahi kuishi Beijing, nchi tajiri yenye uchumi mkubwa lakini kuhama kutoka kwenye matumizi ya mkaa mpaka gesi haikuwa rahisi.
Ilichukua muda, kwanza fedha za kuweka sawa miundombinu muhimu kuwezesha matumizi na nishati hiyo mbadala. Pili ni elimu kwa wananchi, kwa mfano, inahitaji elimu kumwambia mkulima-- chukulia bibi yangu aliye kijijini ambaye amezoea kupika kwa kuni anazozikata shambani kwake-- leo ukimwambia atumie chanzo kingine cha nishati inahitaji kubadili mazoea aliyokuwa nayo. Mikutano kama hii ni sehemu ya majukwaa muhimu ya kubadilishana uzoefu.

Advertisement