Kampeni ya ‘shida mtaji’ yazinduliwa

Muktasari:

  • Kampuni ya Selcom na Mastercard kwa pamoja kupitia huduma yao ya QR Masterpass wamezindua kampeni kwa wafanyabiashara ambayo inatarajia kupunguza matumizi ya fedha tasilimu katika mauzo na manunuzi.
  • -Wakati wa kampeni hiyo kila wiki itachezeshwa droo moja ambapo mfanyabiashara mmoja anayetumia huduma hiyo atashindia Sh1 milioni.

Dar es Salaam. Kampuni ya Selcom na Mastercard kwa pamoja kupitia huduma yao ya QR Masterpass wamezindua kampeni kwa wafanyabiashara ambayo inatarajia kupunguza matumizi ya fedha taslimu katika mauzo na manunuzi mbalimbali.

Kampeni hiyo iliyozinduliwa jana Jumatatu Novemba 19 inahusisha wafanyabiashara wanaotumia huduma hiyo na ambao watajiunga, itakayofanyika kwa miezi mitatu mfululizo ambapo kila wiki mfanyabiashara mmoja atashinda Sh1 milioni.

"Selcom na Mastercard tumeshirikiana kuleta kampeni hii ambayo tumeiita Shinda mtaji, hii itasaidia kuongeza mtaji wa wafanyabiashara lakini pia kuongeza usalama katika manunuzi kwa kupunguza matumizi ya fedha taslimu katika malipo," amesema Juma Mgori Mkuu wa Masoko wa Selcom Tanzania.

Magori amesema wafanyabiashara wakubwa, wadogo na wakati  ambao bado hawajajiunga na huduma hiyo ni vyema wakachangamkia fursa kwakuwa kwa hali ya sasa Sh1 milioni sio fedha ndogo zinaweza kuboresha biashara kwa kiasi fulani.

Amesema huduma hiyo ya malipo imeunganishwa na benki 12 zilizopo hapa nchini na mitandao yote ya simu inayotoa huduma za miamala na mauzo yote, mauzo ya siku kwa mfanyabiashara  yataingizwa katika akaunti yake moja kwa moja kila siku.

Aidha katika uzinduzi huo droo ya kwanza ilichezeshwa Kampuni ya  GA iliibuka mshindi wa wiki hii.