Kuimarika mapato ya madini kutakanyowanufaisha Geita

Thursday February 14 2019

Shughuli za uchimbaji madini zikiendelea

Shughuli za uchimbaji madini zikiendelea biashara ambayo inaliingiza fedha nyingi Halmashauri ya Geita. Picha ya Maktaba. 

By Mussa Juma, Mwananchi [email protected]

Mabadiliko ya Sheria ya Madini yaliyofanywa na Serikali mwaka 2017, yameanza kuonyesha tija mkoani Geita ambako mapato yameongezeka hivyo kuupa nafasi ya kupanga namna ya kuwanufaisha wananchi.

Kwenye taarifa ya Serikali iliyobainisha ukusanyaji wa mapato katika halmashsuri zote nchini iliyotolewa na Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jafo mwaka jana, ilionyesha ufanisi wa halmashauri ya Mji wa Geita ulivuka malengo.

Taarifa hiyo ilibainisha mapato ya halmashauri yalifika asilimia 218 ikifuatiwa na halmashauri ya Wilaya ya Kibaha iliyopata asilimia 165 na Mpimbwe asilimia 162 wakati Halmashauri ya Mbinga (asilimia 20), Songea (asilimia 33) na Halmashauri ya Rorya (asilimia 37) ndizo zilizokusanya kiasi kidogo zaidi ya kilichopangwa.

Licha ya halmashauri hiyo kuongoza kwa makusanyo kitaifa, Mkoa wa Geita ulikuwa miongoni mwa mikoa mitatu iliyovuka malengo ya ukusanyaji ikipata asilimia 104 hivyo kuungana na Dodoma (asilimia 170) na Njombe (asilimia 103).

Ikiwa na wilaya tano ambazo ni Geita, Chato, Bukombe, Mbongwe na Nyang’hwale; Mkoa wa Geita ndio unaoongoza kwa uchimbaji wa dhahabu kwani mgodi mkubwa zaidi unaosimamiwa na kampuni ya Geita Gold Mine (GGM) upo humo.

Kujitofautisha na Mkoa wa Shinyanga unaoongoza kwa uchimbaji wa almasi nchini ukiwa Mgodi wa Mwadui huku ukikabiliwa na umasikini, Geita imeamua kuweka mikakati ya kubadilisha kilichoshindikana huko ili kuwanufaisha wananchi na rasilimali zilizopo katika ardhi yao.

Mkurugenzi wa Mji wa Geita, Method Apolinary anasema haiwezekani wananchi wanazaliwa katika maeneo yenye utajiri wa madini ila wao wanabaki masikini.

Mhandisi huyo wa madini anasema walikubaliana kuibadili Geita kwa kuboresha huduma za kijamii, afya, elimu na maji kwa kuweka mikakati itakayowanufaisha wananchi.

Apolinary anasema baada ya Serikali kufanya mabadiliko ya Sheria na Madini mwaka 2017 ambayo iliwataka wawekezaji wa dhahabu kutoa asilimia 0.7 ya mapato ghafi kwa halmashauri walimowekeza, wao walienda mbali zaidi.

Kwa fedha walizopokea kutoka Mgodi wa GGM, anasema walianza kutekeleza miradi ya maendeleo kwani baada ya mabadiliko hayo ya sheria, kwa mara ya kwanza, walipokea Sh9.2 bilioni.

“Hivi sasa tunakwenda vizuri na ndio sababu sasa tunatajwa kama moja ya halmashauri makini nchini kutokana na uwezo wetu mkubwa wa ukusanyaji mapato lakini tuna miradi mikubwa ambayo inaonekana,” anasema.

Ili kuwashirikisha wananchi kwenye mapato hayo, Apolinaly anasema wanajenga soko la kimataifa ambalo litakalogharimu zaidi ya Sh2 bilioni kulikamilisha.

Pamoja na soko hilo, kuna ujenzi wa viwanda vya kuchenjua dhahabu unaendelea, ujenzi wa shule mpya za msingi na sekondari na jengo la halmashauri ambavyo vinatarajiwa kuongeza tija mkoani humo.

Mweka hazina wa Mji wa Geita, Munguabela Kakwilima anasema ujenzi wa soko ukikamilika, litakuwa na jumla ya vizimba 1,000 na maduka yatakayoiingizia halmashauri zaidi ya Sh300 milioni kwa mwaka.

“Huu ni mkakati wa kukuza uchumi wa wananchi, hivyo tunataka katika soko hili huduma zote zipatikane ikiwamo benki, maduka ya jumla na huduma nyingine muhimu,” anasema Munguabela.

Kukamilika kwa mipango yote inayoendelea kutekelezwa mkoani humo, uongozi unaamini takriban watu 192,000 waliomo watagushwa na miradi mipya ya kiuchumi iliyoanzishwa.

“Tunataka wauzaji wa madini wafanye biashara na viwanda ambavyo tumeanzisha vifanye kazi bila matatizo kwani kuna malighafi za kutosha,” anasema.

Mwenyekiti wa Halmasauri ya Geita, Leonard Bugomola anasema kutoka kwenye viwanda vya uchenjuaji madini ya wachimbaji wadogo wameanza kukusanya ushuru tofauti na miaka ya nyuma.

“Kuna viwanda vidogo 14 vya kuchenjua dhahabu ambavyo kwa mwezi tunakusanya Sh40 milioni. Viwanda hivi ni sehemu muhimu ya mapato ya halmashauri na vinasaidia kutoa ajira kwa vijana,” anasema.

Licha ya ushuru kwa halmashauri, Mgodi wa GGM pia hutoa fedha kusaidia jamii kupitia kitengo chake cha wajibu kwa jamii (CSR).

Mchumi wa halmashauri hiyo, Emmanuel Malima anasema wamepokea Sh4.9 bilioni ambazo wamepanga kujenga zahanati, shule na vituo vya afya.

“Tuna miradi 14 ya majengo ya zanahati na vituo vya afya na ujenzi wa shule ambapo zaidi ya Sh1.5 bilioni zitatumika,” anasema mchumi huyo.

Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Apolinary anasema katika kupanga matumizi ya fedha zinazokusanywa kutoka vyanzo tofauti, anasema wamepanga kutumia sehemu ya fedha hizo kuweka taa za barabarani, kujenga shule mpya 10 za msingi na tano za sekondari.

Licha ya maeneo hayo, meneja wa Wakala wa Barabara Mjini na Vijijini (Tarura) wilayani Geita, Patrick Chadu anasema mwaka huu wamepanga kutumia zaidi ya Sh1.6 bilioni kuboresha barabara ya mjini.

Wananchi

Peter Ndaki ni mfanyabiashara wa madini anasema tangu kuanzishwa viwanda vya uchenjuaji uzalishaji umeongezeka lakini changamoto ni gharama kubwa. Ili kuongeza uzalishaji wao, anaiomba Serikali kuangalia namna ya kupunguza kodi na tozo zilizopo kwenye sekta hiyo. “Tunaweza kuongeza uzalishaji kama serikali ikitupunguzia kodi, madini yapo lakini kodi na gharama za kuchenjua ni kubwa,” anasema.

Ines Fumbo mkazi kijiji cha Nyamakale anasema ujenzi wa soko la kisasa utawapa faraja kwa kwa kuwawezesha kufanya biashara saa 24.

“Unapokuwa na muda wa kutosha kufanya biashara, mapato yako yanaongezeka. Soko litafungua fursa nyingine kwetu,” anasema.

Advertisement