Kwa nini vijana wajiajiri katika kilimo, ufugaji?

Monday May 20 2019

 

Kilimo ni uti wa mgongo wa Tanzania na ndiyo sekta iliyoajiri watu wengi, zaidi ya asilimia 60.

Inakadiriwa kila mwaka vijana 800,000 wanaingia kwenye soko la ajira wakitokea shule za msingi, sekondari, vyuo vya kati na vikuu wakisaka ajira rasmi na zisizo rasmi. Ili vijana wajiajiri kwenye kilimo chenye tija, wanahitaji kuwezeshwa mitaji na mafunzo.

Mwandishi Wetu Elias Msuya amefanya mahojiano na mkurugenzi wa Shirika Uwezeshaji Kilimo (PASS), Nicomed Bohay, kuhusu mpango wa kudhamini mikopo kwa wajasiriamali nchini ili kujikwamua na umaskini. PASS ilianzishwa mwaka 2000 chini ya programu ya kusaidia sekta ya kilimo ili kuwezesha upatikanaji huduma za fedha na biashara kwa wajasiriamali wa bidhaa na huduma katika sekta ya kilimo nchini

Swali: Mitaji ni tatizo sugu la wajasiriamali wa kilimo. PASS imewezaje kuwakomboa?

Jibu: Tangu PASS ilipoanzishwa, tumewanufaisha wajasiriamali wa kilimo 929,172 waliopewa mikopo ya Sh712 bilioni na benki kwa udhamini wetu. Mwaka 2018, ilinufaisha biashara 196,873.

Mwaka huohuo tulidhamini mipango ya biashara 15,564 yenye thamani ya Sh191 bilioni iliyowasilishwa kwenye benki tunazoshirikiana nazo. Kwa kuwa PASS si benki, tunashirikiana na benki za biashara kutoa mikopo hiyo na sisi tunaidhamini tu.

Advertisement

Swali: Mnawasaidiaje wakulima vijana kufaidika na mikopo?

Jibu: Tunayo atamizi chini ya ubunifu wa kilimo (AIC) ambayo iko Morogoro ambayo hutoa mafunzo ya kilimo cha biashara. Tunajua kuna vijana wapatao 800,000 wanaingia kwenye soko la ajira kila mwaka, ndiyo maana tumeanzisha atamizi hiyo.

Swali: Kuna miradi mingine ambayo PASS inajivunia?

Jibu: Katika atamizi kuna vijana 20 katika nyumba 20 wanaofundishwa uzalishaji nyanya tangu upandaji, kuweka mbolea, matunzo, uvunaji, kuweka kumbukumbu, kufanya miamala benki, bajeti, mauzo na masoko.

Swali: Baada ya mafunzo hayo, vijana hao mnawapeleka wapi, au wanarudi mitaani?

Jibu: Baada ya mafunzo ya mwaka mzima, hutafutiwa ardhi ili waendelee na kilimo, pia huwasaidia kupata mikopo benki kwa dhamana ya asilimia 80.

Advertisement