Maandalizi ya maonyesho ya sabasaba yapamba moto

Wednesday June 26 2019

Maandalizi ya maonyesho ya 43 ya biashara ya

Maandalizi ya maonyesho ya 43 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yakiwa katika hatua za mwisho yanayotarajia kuanza kesho kutwa ijumaa katika viwanja vya Jk Nyerere Barabara ya Kilwa jijini Dar es Salaam. Picha na Anthony Siame 

By Aurea [email protected] [email protected]

Dar es Salaam. Siku moja kabla ya kuanza kwa maonyesho ya 43 ya kimataifa ya biashara ya sabasaba jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, baadhi ya washiriki wameanza kusogeza bidhaa zao kwa ajili ya kuweka katika mabanda.

Mbali na washiriki pia vijana wengi wamejitokeza kutafuta nafasi za ajira za muda ili kujiingizia kipato huku watu wa mapambo wakichangamkia fursa za upambaji.

Maonyesho hayo yanayoratibiwa na Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (Tantrade) yataanza keshokutwa Ijumaa Juni 28 – Julai 8, 2019.

Mwananchi ilifika leo Jumatano Juni 26, 2019 katika viwanja vya maonyesho vya Mwalimu Julius Nyerere na kujionea shughuli za upambaji zikiendelea katika mabanda pamoja na pilikapilika za kusogeza  bidhaa kwenye maonyesho hayo.

Akizungumza mmoja wa wapambaji na mkazi wa Mbezi Beach, Asha Saidi amesema maonyesho hayo yamekuwa yakiwaingizia kipato kikubwa kila msimu wa sabasaba unapofika.

“Mara nyingi huwa nina mawasiliano na baadhi ya ofisi za umma hivyo kila msimu unapofika huwa wananitafuta nakuja kuwapambia,” amesema Asha

Advertisement

Mmoja kati ya vijana wanaotafuta ajira katika maonyesho hayo, Jumanne Jumanne amesema ni mara yake ya nne kutafuta ajira ya kufanya katika maonyesho hayo tofauti na kukaa nyumbani.

“Kuna kampuni huwa naisaidia kutangaza biashara zao katika maonyesho haya hivyo huwa najipatia Sh10,000 kwa siku pamoja na hela ya nauli hivyo huwa sijutii kufanya nao kazi badala ya kukaa nyumbani,” amesema Jumanne

 

Lailat Mussa ambaye ni mmoja wa wafanyabiashara amesema amefika leo katika mabanda hayo ili kuangalia hali ilivyo kabla hajafikia uamuzi wa kuweka mapambo.

“Nilikuja kuhakikisha kama banda langu limewekwa namba na jina la utambulisho wa bidhaa yangu ili kuweka mapambo maana kesho itakuwa ni purukushani ya kuleta vitu.” amesema Lailat ambaye ni muuzaji wa bidhaa mbalimbali za asili

Ofisa Mahusiano wa TanTrade, Theresia Chilambo alipoulizwa juu ya idadi kamili ya wafanyabiashara waliojisajili kushiriki maonyesho hayo ameomba kusubiriwa mkutano wa Waziri wa Viwanda, Biashara ndiyo utakaokuwa na majibu yote bila kubainisha utafanyika siku gani.

Lakini awali akizungumza na Mwananchi Ijumaa ya Juni 21, 2019 alibainisha zaidi ya kampuni 2000 kutoka nchi zaidi ya 35 zilikuwa zimethibitisha kushiriki na usajili ulikuwa ukiendelea.

Advertisement