Mashabiki wa Simba, Yanga wapunguza kula siku za mechi

Muktasari:

  • Ushindi wa timu kubwa nchini huwa neema pia kwa wafanyabiashara waliopo jirani na Uwanja wa Taifa hata kwingineko mfano Kariakoo. Hali ilikuwa hivyo na wajasiriamali walipenda mechi ichezwe hata kila mwezi. Lakini kwa siku za karibuni, mapato yao yameshuka na waathirika wakubwa zaidi ni wauzaji wa vyakula.

Katika mechi mbili mfululizo ambazo Simba imecheza na kushinda katika Uwanja wa Taifa na kuwafurahisha mashabiki wao, wajasiriamali waliokuwa wananeemeka kila mechi kubwa inapochezwa, wanalia njaa.

Wajasiriamali hao wanasema siku za nyuma, ilikuwa neema lakini siku za hivi karibuni hali imebadilika, biashara imeshuka. Wanaolalamikia hali hiyo zaidi ni wauzaji wa chakula jirani na Uwanja wa Taifa.

Ilikuwa kawaida siku za nyuma kwa baa zilizo maeneo hayo kujaa mashabiki pindi Simba na Yanga zinapocheza au moja kati ya timu hizo zinazpopambana na nyingine za ligi kuu. Mashabiki hao walifuata chakula na vinywaji.

Kwa sasa, wauzaji wa vinywaji hasa bia mambo hayajabadilika sana lakini wauza chakula wanauona mwenendo usioridhisha.

Muuza chipsi katika Bar ya kwa Chichi anayejulikana kwa jina maarufu kama Tall anasema wanapata riziki kunapokuwa na mechi kubwa lakini mauzo yameshuka.

“Tunashukuru biashara tunafanya kunapokuwa na mechi kubwa tofauti na siku za kawaida lakini si kama ilivyokuwa miaka ya nyuma. Hivi sasa katika mchezo wa Simba na Yanga tunauza gunia moja mpaka moja na nusu wakati zamani tulikuwa tunauza kati ya magunia matatu hadi matano,” anasema Tall.

Muuzaji mwingine wa chipsi katika eneo la kuuzia chakula maarufu kwa mama Omary, Abdul Kassim anasema mechi za Simba na Yanga ulikuwa ukiwanufaisha zaidi siku za nyuma ila miaka ya karibuni watu wamekuwa hawana mwamko wa kununua chakula.

“Kwa kawaida kukiwa na mechi za kawaida tunaweza tukauza hata ndoo nne hadi gunia moja lakini ikiwa Simba na Yanga huwa tunauza hata magunia matano lakini katika mechi iliyopita hata gunia mbili hatukumaliza,” anasema Kassim.

Sio chipsi pekee, hata nishkaki na nyama choma anasema nayo haiendi kama zamani kwani kwa siku huwa wanauza kilo tano za mishkaki lakini kwenye mechi kubwa ni kati ya kilo 15 hadi 20 wakati kuku hufika 50.

Muuza nyama choma wa eneo hilo aliyepo baa iliyo jirani na uwanja huo, Emmanuel Kimario anasema mechi iliyopita ya Yanga na Simba aliuza mbuzi mmoja na nusu na kilo 15 za nyama ya ng’ombe.

“Zamani miaka ya nyuma tulikuwa tunauza kati ya mbuzi wanne hadi watano lakini kwa sasa watu wamekuwa makini hivyo tunauza mbuzi mmojnusu na ikizidi sana wawili na ugali tukipika kilo 10 tu wakati zamani ilikuwa hadi kilo 30,” anasema.

Muuza chipsi katika Baa ya Kipara, Saleh Ally anasema wateja wengi wamepungua kwa sababu ya hali ngumu ya kiuchumi. Kwenye mechi ya watani wa jadi iliyopita anasema alinunua gunia moja akitegemea atalimaliza lakini halikuisha kwani aliuza ndoo nne tu.

“Zamani nilikuwa nauza magunia mawili hadi matatu lakini sasa hivi ni ndoo nne. Watu hawana fedha. Tulikuwa tunauza kati ya kuku 40 mpaka 50 lakini mechi iliyopita nimeuza kuku 20 tu,” anasema Ally.

Anasema hata kilo saba za nyama alinunua kwa ajili ya kuandaa mishikaki hazikuisha tofauti na miaka ya nyuma alipokuwa akiuza mpaka kilo 10 kwenye kubwa ya Simba na Yanga.

Hata wachache wanaojitokeza, anasema wamebadili utaratibu. Wamepunguza mahuitaji ya chakula wanachokihitaji badala ya kuagiza chipsi mayai na mishkaki kadhaa sasa hivi wanapendelea zaidi chipsi kavu.

“Yaani namuomba Rais John Magufuli alegeze kidogo jamani maana watu wamekuwa hawana hela…mteja akija anaagiza chipsi kavu tu na ukimuuzia kwa Sh2,000 analalamika,” anasema Ally.

Kwa kawaida, anasema huwa wanauza chipsi kavu kwa Sh1,500 lakini kwenye mechi ya Simba na Yanga hupandisha mpaka Sh2,000 ili kufukia hasara ya siku za kawaida.

Meneja wa baa ya kwa Kipara, Witnes Kuzwa anasema katika mchezo wa watani wa jadi huwa wanauza bia nyingi zaidi kuliko siku nyingine zote.

“Huwa tunauza sana kwani watu wanakunywa kabla ya kuingia uwanjani hata wanapotoka. Kwa sababu baa yetu ni ndogo tunauza kati ya kreti 10 hadi 20 kwenye mechi hizo,” anasema.

Licha ya bia, Witness anasema vinywaji vikali hasa K Vant huwa inanunuliwa zaidi zinapokutana Simba na Yanga.