Mbegu za maboga zilinitibu sasa zinanipa maisha

Thursday February 14 2019

 

Ni vyema kujiuliza huwa unafanya nini unapofanikiwa kutatua tatizo lililokuwa linakukabili…wapo baadhi ya wajasiriamali wadogo kwa wakubwa wanaoiona fursa kwenye changamoto wanazokutana nazo maishani.

“Niliigundua biashara hii nilipokosa maziwa kwa siku mbili baada ya kujifungua na kumfanya mwanangu apate ugonjwa wa njano,” anakumbuka.

“Nilipewa elimu namna mbegu za maboga zinavyosaidia kuzalisha maziwa kwa akina mama wanaonyonyesha. Nilipojaribu na kuona faida zake nilianza kuutengeneza unga huu ili niwasaidia na wengine.”

Hayo ni maneno ya Dominica Kapande (39) mama wa watoto watatu anayeuza unga wa mbegu za maboga. Anasema alianza biashara hiyo kwa mtaji wa Sh9,000 tu mwanzoni mwa mwaka jana.

Kwa sasa, anafunga unga huo katika uzito tofauti ili kuwaruhusu hata walio mbali kuubeba bila wasiwasi kwenda kuutumia nyumbani.

Licha ya kuuza bidhaa hiyo kwa bei nafuu, Dominica anasema kuna uelewa mdogo wa jamii kuhusu matumizi ya unga huo hivyo kulazimika kuwaelimisha wateja wake kabla hawajaununua.

Pamoja na hali hiyo anaamini ongezeko la wajasiriamali wanaowekeza kwenye mbegu hizo bila litasaidia kufikisha elimu kwa wananchi wengi zaidi.

Kutokana na teknolojia duni anayoitumia, anasema kwenye kila kilo moja ya mbegu hizo anaweza kupata nusu kilo au zaidi kidogo.

“Nafunga wa robo, nusu hata kilo moja. Huwa nauza kwa bei ya jumla au rejareja,” anasema.

Advertisement