MWANANCHI JUKWAA LA FIKRA: Mradi wa kilimo mseto wabadili maisha ya wananchi Singida

Mkoa wa Singida ni kati ya mikoa ya Kanda ya Kati ukiwa pamoja na Dodoma. Hali ya hewa ni ya ukavu ikipata mvua chache na miaka mingine huwa ya ukame kabisa. Kwa ujumla Singida hupata kati ya milimita 500 hadi 800 za mvua kwa mwaka ambazo ni za masika na vuli.

Hali hiyo inaufanya mkoa huo kutozalisha chakula kwa wingi na hivyo kuwaweka wananchi katika hali ya tahadhari ya ugonjwa wa utapiamlo unaoathiri zaidi watoto wadogo.

Mwaka 2016 Taasisi ya Action Aid Tanzania ikishirikiana na Chuo Kikuu cha Cornell cha Marekani na Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Mandela Afrika wamekuwa wakitekeleza mradi wa lishe na kilimo cha mazingira (Singida Nutrition and Agroecology- Snap) ili kusaidia kaya zinazoathiriwa na ukame na mila potofu zinazoathiri lishe katika jamii.

Wakizungumzia mradi huo, unaohudumia vijiji 20 vya halmashauri ya wilaya ya Singida, baadhi ya wanavijiji wanasema wamepata uhakika wa chakula kutokana na mbinu za kilimo mseto walizofundishwa.

“Awali tulikuwa tunalima zao moja tu shamba zima, baadaye tukafundishwa kuhusu kilimo mseto, sasa tunalima mbaazi, mahindi, mtama mdogo, kunde na karanga kwenye shamba moja. Tunapanda kila zao katika mstari wake,” anasema Dominica Juma Mhongo kutoka kijiji cha Msikii.

Anaendelea, “Zamani tulikuwa tunavuna gunia mbili za mahindi kwenye ekari moja, lakini tangu mwaka 2016 tulipoanza kilimo mseto, unakuta shamba moja unatoa kunde debe tatu hadi gunia moja, karanga gunia tatu, maharage gunia moja na mahindi ya kutosha kwa hiyo hakuna ukosefu wa chakula katika nyumba.”

Mwanakijiji mwingine Ally Irumbe anaeleza kuwa mafunzo waliyoyapata kuhusu matumizi ya mimea kama mbolea akisema wameanza matumizi ya mimea ya jamii ya mikunde baada ya kutumia mbolea pekee shambani.

“Mbolea tunayotumia ni ya kawaida, samadi na mboji na mbegu za asili. Lakini mradi ulipoanza tuliambiwa tuchanganye kunde na mazao mengine kwa kuwa inazalisha mbolea” anasema. Irumbe ambaye alikuwa mmoja wa wanavijiji 20 waliopelekwa Malawi kujifunza kilimo mseto, anasema mradi huo umebadilisha mtazamo wa jamii katika uzalishaji mali na lishe.

“Baada ya kutoka kule ndiyo tukaanza kuwafundisha wenzetu kilimo mseto, mpaka sasa ndoa zetu haziyumbi ambapo ilikuwa baba hafanyi kazi anamuachia tu familia na mwingine ni mlevi akija hafanyikazi,” anasema.

Kuhusu ushiriki wa jinsia katika lishe, mwanakijiji Asha Daffi anasema awali hawakujua hata jinsi ya kulisha watoto jambo lililokuwa likisababisha utapiamlo kwa watoto hao.

“Tulikuwa tukiwapa uji watoto wakiwa na umri wa miezi miwili, kumbe tunatakiwa kuwanyonyesha hadi wafikie miezi sita. Wanaume walikuwa hawasaidii kazi za nyumbani wala shambani. Yaani ukiwaacha watoto na baba yao ukirudi utakuta wameshinda njaa, lakini kwa elimu tuliyopata sasa wanaume wanalisha watoto,” anasema.

Mbali na kilimo mseto na masuala ya jinsia, wakulima pia wamejifunza jinsi ya kutuimia miti dawa kukinga mimea isishambuliwe na wadudu.

Irumbe anasema kwa sasa wanatumia zaidi mti wa mfaranjovu wenye harufu kali inayoogopwa na wadudu.

“Ule mti una harufu kali sana. Unauweka ndani ya maji halafu unanyunyizia kuzunguka shamba zima, unasaidia. Tumejaribu, bangi ya mwa, ndulele, mwarobaini, lakini bado mazao yalikuwa yanaliwa. Kuna wadudu wanapekecha mimea na kuingia ndani kiasi kwamba hata ukipiga dawa hawaathiriki,” anasema na kuongeza: “Dawa hizi zimetusaidia tu kwa kiasi fulani kuliko kuacha kabisa. Dawa za kemikali hatujatumia kwa sababu tuliambiwa zinaharibu mazingira na wadudu rafiki wa mimea. Unaweza kuua nyuki au kipepeo ambao wanachavusha ule mmea.”

Akifafanua zaidi kuhusu miti hiyo, mwanakijiji Rashid Omari anasema miongoni mwa mimea wanayotumia ni pamoja na mwarobaini na bangi ya mbwa, ndulele na aloevera.

“Unachukua Aloevera, mwarobaini, bangi ya mbwa na ndulele unachanganya na kuloweka kwenye maji kisha unaacha saa 24. baada ya hapo unakamua na kisha maji yake ndiyo unaweka kwenye bomba kwa ajili ya kupulizia shambani,” anasema.

Hata hivyo, mwanakijiji Ally Khamis ameonya matumizi yaliyopita kiasi ya mti wa mfaranjofu akisema yanaweza kuitowesha miti hiyo kama tahadhari isipochukuliwa.

Profesa mshiriki wa Chuo Kikuu cha Cornell cha Marekani Rachel Bezner Kerr kinacholea mradi huo anasema mradi huo ulianza nchini Malawi miaka 20 iliyopita, hivyo waliwapeleka wanavjijiji wa Singida ili wapate uzoefu.

“Tumeona mabadiliko makubwa hasa katika upatikanaji wa chakula na lishe kwa watoto ambao hawakupata chakula cha kutosha. Tumeona mabadiliko hasa katika mbinu za kilimo kwa kuwabadilisha katika kutumia viuatilifu vya kemikali na kutumia miti ya asili, kilimo mseto na matumizi ya mbegu za asili.

“Tumeona pia mabadiliko katika usawa katika jinsia hasa kwa kuwa wanawake walikuwa wakishiriki zaidi kazi za kilimo lakini sasa wanaume nao wanawasaidia katika kazi hizo. Vilevile tumeona mabadiliko ya afya ya akili kwani awali kulikuwa na tatizo la msongo wa mawazo kwa kutokuwa na uhakika wa chakula katika familia,” anasema Profesa Kerr.

Akifafanua mafanikio hayo, mhadhiri katika taasisi ya Sayansi ya Teknolojia ya Mandela, Dk Haikael Martin anasema wakati mradi unaanza kulikuwa na hali duni ya lishe, lakini baada ya kuwafundisha jinsi ya kupata protein mabadiliko yameanza kuonekana.

“Mradi huo umesaidia kukuza kilimo endelevu cha uzalishaji wa mazao ya chakula kwa kaya mara 3.7 kwa kusisitiza uzalishaji wa mazao ya mikundekunde. Mradi pia umeongeza uzalishaji wa kilimo mseto kwa asilimia 43 na ongezeko la matumizi ya miti dawa (botanicals pesticides) kwa asilimia 11. Kwa hiyo mradi umesaidia uhakika wa chakula tofauti na zamani ambapo nusu ya nyumba zilizoko kwenye mradi watu walikuwa wakilala njaa na wengine wakiomba chakula,” anasema Dk Haikael.

Anasema mradi huo pia umesaidia wanandoa na familia kwa jumla kusaidia katika kazi za shamba katika msimu wa kilimo. Wanaume wamekuwa wakiwasidia wake zao kazi za shamba na nyumbani ikiwamo kulea watoto dakika 35 zaidi kwa siku.

Anasema pia mradi huo umewasaidia wanawake waliokuwa wakiteseka kwa msongo wa mawazo kwa asilimia 33 kwa kupunguza vipigo asilimia 50.

“Mradi pia umesaidia lishe kwa watoto kwa kuongeza ulaji wa mazao ya protein. Wakati wa mavuno watoto wa kwenye kaya za mradi wana uhakika wa kula mara 1.8 mazao ya mikundekunde na wana uhakika wa kula mara 2.3 mazao yatokanayo na wanyama kama mayai, maziwa na nyama,” anasema Dk Haikael. Ofisa Kilimo wa wilaya ya Singida (Daico), Abel Mngale mafanikio yaliyoonekana ktaika vijiji 20 yanatakiwa kusambazwa katika vijiji vingine 64 violivyobaki.

“Tuna vijiji 84, kwakuwa tumepata wataalamu kwenye vijiji 20 tutawatumia kuendeleza. Tutaendelea kutenga bajeti yavkililo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa ikiwa pamoja na jinsia na lishe,” anasema.

Hata hivyo anasema changamoto iliyopo kwa sasa ni ufinyu wa bajeti ya maendeleo ambapo anasema tangu mwaka 2015 Serikali haijawahi kutoa bajeti ya maendeleo na hivyo kutishia maendeleo ya miradi huo unaolenga kuvifikia vijiji vingi zaidi.

Akizungumzia mradi huo, meneja wa kilimo na ardhi wa taasisi ya Action Auid Tanzania, Elias Mtinda anasema tangu mradi huo uanze kutekelezwa mwaka 2016 umeonyesha mafanmikio makubwa.

“Tunaiomba Serikali hasa Halmahsauri ya Wilaya ya Singida pamoja na Wizara ya Kilimo kuongeza bajeti ili kuendeleza kile wananchi walichojifunza,” anasema Mtinda