Profesa Sua aishauri Serikali kujikita kwenye kilimo

Wednesday November 14 2018

 

By Bakari Kiango, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kilimo (Sua), Profesa Raphael Chibunda amesema sekta ya kilimo ni njia nzuri itakayosaidia Taifa kufikia azma ya uchumi wa viwanda.

Amesema bado asimilia 70 ya Watanzania wanategemea kilimo na sekta hiyo itasaidia kuzalisha malighafi zitakazotumika kwenye viwanda hivyo.

Profesa Chibunda ametoa kauli hiyo leo, Jumatano Novemba 14, 2018 katika kongamano la kumbukumbu ya Mwalimu, Julius Nyerere lililokuwa na mada inayosema ‘Mtazamo wa Mwalimu Nyerere kuhusu Elimu ya Juu’.

Kongamano hilo lilifanyika Chuo Kikuu cha Mzumbe mkoani Morogoro na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali akiwamo Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula.

Akizungumza sekta ya kilimo, Profesa Chibunda amesema Tanzania imebarikiwa katika sekta hiyo kwa kuwa na hekta milioni 7 za kilimo kati yake milioni 2 zinaweza kutumiwa kwenye kilimo kwa ufanisi.

“Kilimo kitasaidia kuzalisha fedha za kigeni na kitazalisha viwanda vingine. Ni vema Taifa likajikita katika sekta hii ili tufikie azma ya uchumi wa viwanda,”amesema Profesa Chibunda.

Hata hivyo, Profesa Chibunda amesema ili kilimo hicho kifanikiwe ni vema wakulima wakalima kwa ufanisi kwa kuongeza ukubwa wa mashamba yao na matumizi ya mbegu bora zenye tija zitakazotoa bidhaa mazao bora zitakazotumika kwenye viwanda hivyo.

 

Advertisement