RTO Dodoma awakumbusha madereva kutotumia Pombe wakiwa barabarani

Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Dodoma (RTO) ACP Nuru Selemani akitoa maelekezo kwa dereva bodaboda Noel Mazengo wakati wa ugawaji wa vifaa vya usalama barabarani (Refleectors) ziizotolewa na Kampuni ya bia ya Seregeti kupitia kampeni yake ijulikanayo kama ‘Usinywe na Kuendesha Chombo cha Moto’ iliyozinduliwa jana Ijumaa Mkoani humo.

Dodoma. Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL) imeendesha kampeni yake ya unywaji kiistarabu kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kitengo cha usalama barabarani hapa Mkoani Dodoma, makao mapya ya Serikali huku madereva wakinufaika na vifaa vya usalama barabarani.


Kampeni hiyo maarufu kama ‘Usinywe na Kuendesha Chombo cha Moto’ imelenga kuwafikia watu 1,000 wakiwamo madereva hususan bodaboda, wanafunzi wa vyuo pamoja na umma kwa lengo la kutoa elimu juu ya unywaji kiistarabu ili kupunguza ajali zitokanazo na ulevi.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika jana katika Hoteli ya Morena jijini hapa, Mkurugenzi wa Uhusiano wa SBL, John Wanyancha alisema kampeni hiyo imelenga katika utoaji elimu kwa wateja wake nchini ili kupunguza matukio yanayoepukika kama ajali zitokanazo na unywaji wa pombe kupindukia.


“SBL imejidhatiti katika kuunga mkono juhudi za Serikali, watu binafsi, wadau na makampuni kuhakikisha kwamba jamii hasa madereva ambao kwa kiasi kikubwa ndiyo waathirika wa ajali zitokanazo na ulevi, wanazingatia unywaji kiistarabu kwa usalama wao na abiria,” alisema Wanyancha.


Kampeni hiyo inashirikisha wadau mbalimbali ikiwamo Jeshi la Polisi-Kikosi cha usalama barabarani, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (Sumatra), madereva bodaboda pamoja na jamii kwa ujumla ikilenga katika kupunguza ajali zitokanazo na ulevi wa kupindukia nchini.


Kwa upande wake,Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma (RTO) ACP Nuru Selemani amesema kampeni hiyo ni chachu katika kupunguza ajali huku akiwataka madereva kuzingatia elimu iliyotolewa ili kuongeza usalama wao wawapo barabarani.


“Kulishirikisha jeshi la polisi, kikosi cha usalama barabarani, kunaonyesha ni kwa jinsi gani SBL wanatilia maanani suala zima la usalama barabarani hasa matokeo ya ulevi na uendeshaji vyombo vya moto. Uzoefu unaonyesha kwamba baadhi ya watu hujisahau na kujiingiza katika ulevi wa kupindukia bila kuzingatia usalama wao na wa vyombo vya moto wanavyoendesha”. alisema.

Kwa mujibu wa ripoti za Jeshi la Polisi-Kikosi cha Usalama barabarani kwa mwaka 2018, jumla ya ajali 876 za bodaboda ziliripotiwa kutokea na kusababisha vifo 366 na majeruhi 694. Ripoti zinaonyesha kupungua kwa ajali hizo ambapo kwa mwaka 2017 zilikuwa 1,459 zilizosababisha vifo 728.


Ili kupambana na ajali hizo, SBL imekabidhi jumla ya makoti ya usalama barabarani (Reflectors) 80 kwa madereva bodaboda ili kuhimiza uzingatiaji wa sheria za usalama barabarani.


RTO aliwataka madereva kutumia makoti hayo ipasavyo kila wanapokuwa katika majukumu yao ya kila siku kwa usalama wao, abiria na watumiaji wengine wa barabara.