Rwakatare akopesha wanawake Sh37 mil

Monday June 11 2018

 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Kilombero. Mbunge wa Viti maalumu (CCM), Getrude Rwekatare amekopesha Sh37 milioni kwa vikundi 185 vya wanawake katika majimbo ya Kilombero na Mlimba ili wajikwamue na umaskini.

Rwakatare alisema mikopo hiyo inayotolewa kila kata wilayani Kilombero, inalenga kumuendeleza mwanamke ili ajitegemee kiuchumi.

“Tulianza kutoa mikopo hii kwa kata 51 za Ifakara zilizopata Sh10.2 milioni. Tarafa za Mang’ula na Kidatu kuna vikundi 65 vilivyokopa Sh13 milioni na Jimbo la Mlimba vikundi 69 vilivyopata Sh13.8 milioni. Kuna kata tano hazijapewa fedha,” alisema.

Rwakatare aambaye pia ni mchungaji alifafanua kuwa kila kikundi kilikopeshwa Sh200,000 na baada ya miezi miwili kinatakiwa kurejesha Sh210,000.

Naye mratibu wa mafunzo ya ujasiriamali na mikopo hiyo, Hadija Lifulama alisema baada ya vikundi hivyo kupata mkopo huo vinatakiwa kurejesha mapema ili viweze kupata mara mbili yake ili kufanikisha biashara zao.

“Hakuna mwanamke mshamba kwenye maendeleo. Usichukue mkopo na kununua dera ili uonekane wa leo. Maendeleo huja kwa mwanamke asiyebagua kazi ya kufanya kujipatia kipato,” alisema.

Advertisement