Serikali inavyojipanga kumaliza uhaba wa chanjo za mifugo nchini

Thursday February 7 2019

 

By Julius Mnganga, Mwananchi [email protected]

Ingawa Tanzania ni miongoni mwa nchi zinazoongoza Afrika kwa wingi wa mifugo, ni Botswana ndiye kinara wa kufasirisha nyama ughaibuni ingawa ina ng’ombe milioni nne tu.

Takwimu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zinaonyesha kuna zaidi ya ng’ombe milioni 31, mbuzi milioni 30 na kondoo milioni 10. Vilevile, kuna zaidi ya kuku milioni 38 wa kienyeji na milioni 36 wa kisasa wanaofugwa kwa ajili ya nyama au mayai.

Tofauti na nchi nyingine duniani, ufugaji wa Tanzania ni wa kienyeji unaokabiliwa na magonjwa hasa wafugaji wadogo.

Mkurugenzi wa huduma za mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Dk Hezron Nonga anasema kuna udhaifu katika mfumo wa uchanjaji nchini ila ni suala linalofanyiwa kazi ili kuongeza tija kwa wafugaji.

“Tunatarajia kuuzindua muongozo wa uchanjaji nchini ambao utabainisha wazalishaji, waingizaji na wasambazaji wa chanjo nchini. Hii itasaidia kudhibiti magonjwa hivyo kuongeza ubora wa nyama na bidhaa nyingine za mifugo,” anasema Dk Nonga.

Miongoni mwa sababu za wafugaji wengi kutochanja mifugo yao ni gharama kubwa za chanjo husika pamoja na ubora.

Samson Makweta, mkazi wa jijini Dar es Salaam anasema amewahi kuhangaika kuwatibu mbwa wake kwa muda mrefu. “Nina mbwa watatu ambao wakati fulani walikuwa na kupe. Niliwatibu kwa zaidi ya dozi tatu. Dawa za mwanzo hazikusaidia kabisa,” anasema Makweta.

Hester Biosciences Africa

Kati ya wawekezaji walioingia nchini siku za hivi karibuni ni Hester Biosciense Africa inayotarajia kuzalisha chanjo tofauti za mifugo.

Mkurugenzi wa kampuni hiyo nchini, Dara Lakdawalla anasema kwameichagua Tanzania kuwa kitovu cha usambazaji wa bidhaa zao barani Afrika.

“Tupo kwenye hatua za mwanzo za ujenzi wa kiwanda. Kitakapokamilika tutakuwa na uwezo wa kuzalisha dozi bilioni mbili kwa mwaka. Asilimia 20 itauzwa nchini na kiasi kinachobaki kitasambazwa kwingineko Afrika,” anasema Lakdawalla.

Kwa sasa, anasema wanatengeneza chanjo 39 zikiwamo 12 za kuku na ndege wengine wafugwao.

“Mwaka jana tuliipa Serikali dozi milioni mbili za mdondo au kideri na leo (juzi) tumetoa kiasi kama hicho. Hizi ni chanjo zilizotengenezwa India ila ndizo tutakazozalisha hapa pia,” anasema Lwakdawala.

Mtaalamu wa mifugo na mtaalamu mkazi wa kiwanda hicho kilichowekeza Dola 18 milioni (zaidi ya Sh41.4 bilioni), Dk Ryoba Kimori anasema kuwawezesha wafugaji wadogo kumudu gharama, wanafunga katika ujazo mdogo ili kupunguza bei.

“Kuna dozi inayowatosha kati ya kuku mmoja mpaka 200 na nyingine inaenda mpaka kuku 500 tofauti na mazoea yaliyokuwapo ya dozi ya kati ya kuku 500 hadi 1,000. Kwa ujazo mdogo, hata mtu mwenye kuku 12 atamudu kununua na kuwakinga na kideri kuku wake,” anasema Dk Kimori.

Kideri au mdondo ni ugonjwa unaosababishwa na virusi ambao husambazwa kwa njia ya hewa hivyo, anasema endapo umeingia nyumba moja ni rahisi kuwafikia kuku waliopo nyumba nyingine.

Kwa mazingira haya, ugonjwa huu huongeza changamoto hata kwa wafugaji wakubwa ambao huwachanja kuku wao endapo wadogo wanaowazunguka hawatawatibu wa kwao.

“Hii ndio mantiki yetu ya kufunga kwa ujazo mdogo ili kila mfugaji aweze kumudu kununua bila kujali wingi wa kuku alionao. Ugonjwa huu ukiingia bandani, kuna uawezekano wa kuku wote kufa,” anasema mtaalamu huyo.

Changamoto dawa za nje

Kama Makweta anavyobainisha kuhusu tiba ya uhakika wa kupe waliokuwa wanawashambulia mbwa wake, Dk Nongo anasema ni kero ya kitaifa kwani amekutano nalo kwenye maeneo alikopita.

Anasema hivi karibuni alikuwa mkoani Kigoma ambako kuna uhamasishaji wa kuogesha ng’ombe ili kukabiliana na kupe pamoja na magonjwa mengine ambako aligundua ukubwa wa changamoto hiyo.

“Alikuja mfugaji akamuweka kupe ndani ya chupa yenye dawa ya kuua kupe lakini kilichotokea, akawa anaogelea humo. Dawa iliyoingizwa haina ubora,” anasema Dk Nongo.

Kukabiliana na changamoto hiyo mkurugenzi huyo amewaomba wazalishaji nchini kutumia vijidudu vinavyotumika kuandaa wa chanjo kutoka nchini vinginevyo wafugaji nchini hawatonufaika ipasavyo na kuboresha mazao yao.

Mkakati

Katibu mkuu wa Wizara ya Mifugo, Profesa Elisante ole Gabriel anasema mkakati uliopo ni kuzalisha chanjo zitakazokidhi mahitaji. Kufanikisha hilo, anasema Serikali itakijengea uwezo kiwanda cha chanjo cha Kibaha (Tanzania Vaccine Institute) kutoka kuzalisha aina nne mpaka aina 10 hapo Januari mwakani.

Licha ya kiwanda hicho cha Serikali, anasema: “Tunaendelea kuhimiza wawekezaji wa sekta binafsi kuanzisha viwanda. Kwa sasa kipo kimoja kinajengwa Kibaha na kampuni ya Hester Biosciences ambacho kinatarajia kuzalisha aina 26 za chanjo kuanzia mwakani.”

Vilevile, anasema kuna mpango wa kuanzisha ununuzi wa pamoja wa chanjo (bulky procurement) utakaosaidia kupunguzi uhaba hata bei za chanjo nchini. Anasema matarajio ni kuwa na viwanda vingi zaidi vitakavyozalisha chanjo tofauti kwa gharama nafuu.

Advertisement