Serikali yatangaza bei mpya ya pamba

Muktasari:

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba (TCB), Marko Mtunga alisema bodi hiyo inatekeleza mikakati ya kuongeza tija kutoka kuzalisha kilo 300 kwa hekari hadi kufikia kilo zaidi ya 1, 000.

Katavi. Msimu mpya wa ununuzi wa pamba umezinduliwa rasmi, huku Serikali ikitangaza bei mpya ya Sh 1, 200 kwa kilo moja ya zao hilo ikiwa ni ongezeko la Sh100 kwa kilo ikilinganishwa na bei ya Sh1, 100 msimu uliopita.

Akizindua msimu mpya wa mauzo ya zao hilo katika kijiji cha Kasekese wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi juzi, Mkuu wa mkoa huo, Amos Makala alisema hakutakuwa na makato yoyote kwenye malipo ya wakulima.

“Serikali inakusudia kuongeza bajeti ya sekta ya kilimo ili kuwahakikishia wakulima upatikanaji wa pembejeo kwa wakati na huduma ya ugani kwa lengo la kuongeza tija na mapato,” alisema.

Aidha, Makala aliutumia fursa hiyo kutangaza mikakati ya kuufanya mkoa wa Katavi kuwa miongoni mwa mikoa inayozalisha pamba kwa wingi, huku akiwaagiza maofisa ugani kuhamia vijijini na kwamba tija na ubora wa mazao ya wakulima katika maeneo yao itakuwa miongoni mwa kipimo cha utendaji wao kazi.

“Huu ni msimu wa pili tangu Katavi tuanze kuzalisha pamba. Msimu uliopita tulizalisha tani 525 na msimu huu tunatarajia kuvuna zaidi ya tani 15, 000,” alisema Makala.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba (TCB), Marko Mtunga alisema bodi hiyo inatekeleza mikakati ya kuongeza tija kutoka kuzalisha kilo 300 kwa hekari hadi kufikia kilo zaidi ya 1, 000.

Alisema licha ya changamoto kadhaa, uzalishaji wa pamba nchini msimu huu unatarajiwa kuongezeka hadi kufikia zaidi ya tani 400, 000 kutoka zaidi ya tani 200, 000 msimu uliopita.

Alizitaja miongoni mwa changamoto zanazokwamisha maendeleo ya sekta ya kilimo nchini ni pamoja na kukosekana kwa huduma za ugani kutokana na uchache wa maofisa ugani, kutopatikana kwa wakati kwa pembejeo na zana za kilimo na mtawanyiko usiotabirika wa mvua za msimu.