Taasisi ya naliendelee ilivyojipanga kutengeneza maziwa ya korosho

Thursday May 30 2019

 

By Haika Kimaro, Mwananchi [email protected]

Wakati zaidi ya tani 270,000 zilizovunwa msimu uliopita zikiwa ghalani mpaka sasa, Chuo cha Utafiti (Tari) Naelendele kimevumbua bidhaa mbadala za korosho yanayoweza kumaliza tatizo la masoko ya zao hilo muhimu kwa uchumi wa Tanzania.

Kutokana na kutouzwa kwa korosho nje ya nchi, pamoja na sababu nyingine, ripoti ya kila mwezi ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha uuzaji wa mazao ya biashara nje ya nchi ulipungua kwa Dola 524.9 milioni kwa mwaka ulioshia Machi 2019 baada ya kuuza bidhaa zenye thamani ya Dola 579 milioni ikilinganishwa na Dola 1.1 bilioni za kipindi kama hicho mwaka jana.

Utafiti wa Taasisi ya Naliendele sio tu unalenga kuongeza thamani ya korosho bali bidhaa zitokanazo na zao hilo kwa soko la ndani na kimataifa.

Licha ya mavuno ya korosho, utafiti wa taasisi hiyo umebaini bidhaa nyingine zinazoweza kumuongezea mkulima kipato ukiacha mapato yatokanayo na mauzo ya korosho ghafi.

Kutokana na mabibo ya korosho ambayo wakulima wengi huyatupa kwa kukosa cha kuyafanyia, taasisi hiyo imegundua yanafaa kutengeneza juisi, mvinyo na jam.

Mtaalamu wa kituo hicho cha utafiti, Regina Msoka anasema katika kila kilo moja ya korosho inayokusanywa shambani, mkulima anaacha kilo tisa za mabibo ambayo yana kipato kikubwa yakisindikwa kuliko korosho zenyewe.

Advertisement

Mabibo yanayoachwa, endapo yatasindikwa, anasema yanaweza kutoa mvinyo wa Sh100,000 tofauti na kilo moja ya korosho ambayo bei yake mara nyingi ni kati ya Sh2,400 na Sh4,000.

“Ukipiga hesabu, katika kilo 10 za korosho kuna kilo 90 za mabibo. Mkulima anaweza kupata Sh40,000 kwa kuuza korosho lakini angeweza kuingiza zaidi ya Sh1 milioni kwa kutengeneza mvinyo,” anasema Regina.

Licha ya mvinyo, anasema kilo moja ya mabibo inaweza kutoa nusu lita ya juisi isiyo na ukakasi. Changamoto iliyopo kwa mabibo ni uhifadhi kwani yanahitaji sehemu yenye baridi (cold room). Kwa mazingira ya sasa, wakulima wengi huyakausha na kutengeneza pombe ya kienyeji maarufu kama ulaka.

Kupata mvinyo, Regina anasema unahitaji kusindika mabibo kwa miezi mitatu na kwenye kilo moja inapatikana lita moja. Kupata juisi, ni mchakato wa siku mbili tu.

Siagi na maziwa ya korosho

Baada ya kubanguliwa, korosho huwekwa kwenye madaraja tofauti. Katika hatua hii, vipande vidogo zaidi vya korosho huachwa na kuuzwa kwa Sh10,000 kwa kilo.

Regina anasema vipande hivyo vinaweza kutengeneza siagi ambayo huuzwa Sh20,000 tofauti na Sh10,000 ya kilo moja ya vipande hivyo.

Katika kilo moja ya vipande hivyo anasema inaweza kutoa lita tatu za maziwa ambazo huuzwa kwa Sh25,000. “Haya hayana mzio wala madhara kwa watumiaji tofauti na ya wanyama,” anasema.

Kwa wanaotaka kuzalisha, Regina anasema mashine za juisi zinapatikana Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido) lakini za bidhaa nyingine zinaagizwa ama kutoka India au Ghana.

Baada ya kukamilisha utafiti na kuanza kutengeneza bidhaa hizo, Regina anasema taasisi hiyo inaandaa utaratibu wa kuzalisha kwa kiasi kikubwa ili zisambazwe nchini kote.

“Tunaandaa mpango wa biashara kuanzisha kiwanda hicho. Tumeshapeleka sampuli ya siagi (Mamlaka ya Chakula na Dawa) TFDA wakithibitisha viwango, tutaanza kuisambaza nchi nzima. Kwa sasa tunazalisha chupa 50 kwa siku za ujazo wa milimita 230 ambazo tunaziuza kwa Sh6,000 kila moja,” anasema.

Kaimu mkurugenzi wa taasisi ya Naliendele, Dk Fortunatus Kapinga anasema: “Kutokana na baadhi ya watu hasa watoto kushindwa kutafuna korosho au kuwa na mzio (allergy) wa maziwa ya ng’ombe, maziwa ya korosho ni suluhisho kwao.”

Wakulima

Mmoja wa wakulima wa korosho mkoani Mtwara, Elisha Millanzi anasema kwa msimu mmoja, anaweza huvuna kati ya tani mbili hadi tatu na mabibo yanayopatikana huyachoma shambani baada ya kukamua juisi kwa machache wanayoweza.

Baadhi ya watu, anasema huyatumia kutengenezea ulaka na wachache hutengenezea pombe haramu ya gongo.

“Serikali ikituletea viwanda vya kutengeneza bidhaa nyingine itakuwa imetusaidia kwa sababu tunatupa rasilimali nyingi. Ukivuna tani 10 za korosho, kumbuka kila korosho ina bibo lake maana yake hapo kuna mabibo tani 10 au zaidi,” anasema Millanzi.

Kwa ajili ya utafiti, malighafi zinazotumika kutengeneza mvinyo, jam na juisi hupatikana kwenye mashamba ya taasisi hiyo huku korosho zinazotengeneza maziwa zikikusanywa kutoka kwenye kiwanda kilichopo ndani ya taasisi hiyo.

Endapo uzalishaji mkubwa utaanza, Regina anasema wakulima watapata soko la mabibo na korosho pia.

Advertisement