Tozo huduma za benki zaongezeka asilimia 50

Tuesday January 22 2019

 

By Ephrahim Bahemu [email protected]

Dar es Salaam. Watanzania wataanza kulipa gharama kubwa zaidi ili kupata huduma za benki baada taasisi hizo za fedha kutangaza kupandisha ada ya huduma kwa asilimia 30 hadi 50.

Kuanzia Februari baadhi ya benki ili kuweza kutoa kiwango fulani cha fedha, lazima akaunti iwe na fedha ya ziada kati ya Sh4,720 hadi Sh6,500 kulingana na aina ya akaunti.

Hali hii inakuja wakati faida ya benki nyingi ikizidi kushuka, huku sekta ya taasisi za fedha ikipambana na mikopo chechefu (NPLs).

Vilevile ripoti za benki kubwa kama NMB, CRDB, Standard Chartered, Exim, TPB zinaonyesha faida yao kupungua kwa mwaka 2018

Wachambuzi wa masuala ya benki wanasema hatua ya benki hizo kupandisha viwango vya utoaji huduma, ni jibu la anguko hilo na kwamba benki nyingi zimeongeza ada za huduma mbalimbali ili kufidia hasara iliyopatikana.

Tangu mwaka 2018 benki nyingi zikiwamo NMB Bank Plc, CRDB Bank Plc, BancABC, Ecobank, PBZ na NBC zilitangaza punguzo la riba kwa wakopaji kwa mikopo binafsi.

Tafsiri ya ongezeko

Hali hiyo inaonyesha kuwa wateja watalazimika kulipa zaidi watakapotoa fedha kwenye ATM au kuulizia salio au kutuma fedha kwa njia nyingine za malipo.

Pia, hali hiyo itawakatisha tamaa wateja wanaotumia mashine za kutolea fedha za benki nyingine kutoa na kutuma fedha kwani ada imeongezwa kwa asilimia 50.

Kwa benki ya NMB kujua salio katika tawi (Kaunta) gharama ya sasa ni Sh2,300 na Sh6,500 kutoa fedha kutoka kaunta kutoka Sh4,012 ya awali.

Wateja wa CRDB nao watalipa kati ya Sh4,720 na Sh6,000 kutoa fedha kaunta kwa akaunti za akiba na amana, gharama za sasa kwa benki hiyo ni kati ya Sh3,540 na Sh4,720 kwa akaunti hizo.

Kutoa fedha kwenye ATM kwa benki ya NMB ni Sh1,150 kutoka Sh944 ya awali, huku mteja wa CRDB akilipa Sh1,200 kwa ATM za benki hiyo kutoka Sh944 lakini kwa wasiokuwa wateja wa benki hiyo watalipa Sh8,000 kutoa fedha.

“Kulingana na idadi kubwa ya wateja wa benki hizo mbili nchi nzima, mkakati huo utawasaidia kuziba mapengo ya kupunguza riba za mikopo binafsi na mikopo chechefu,” alisema mtaalamu wa biashara, Sebastian Kingu alipozungumza na gazeti dada la The Citizen.

Hata hivyo, Kingu alisema chanzo cha mapato katika benki kitaendelea kuwa riba za mikopo kwa wakopaji wake.

Pia, sekta ya benki ilipata jumla ya faida ya Sh426 billioni kwa mwaka 2014 huku mwaka 2015 faida ikipanda hadi 438 bilioni.

Hata hivyo, faida hiyo ilishuka hadi Sh423 bilioni mwaka 2016 na Sh286 bilioni 2017.

Advertisement