Ushindani wa soko wanufaisha wateja, Halopesa yaondoa makato

Friday August 24 2018Naibu mkurugenzi wa Halotel, Nguyen Van Son

Naibu mkurugenzi wa Halotel, Nguyen Van Son 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi [email protected]

Dar es Salaam. Kampuni ya Halotel imetangaza kuondoa gharama za kutuma fedha huku ikiwazawadia muda wa maongezi wateja watakaoweka fedha kwenye akaunti zao.

Akizindua mpango huo, naibu mkurugenzi wa Halotel, Nguyen Van Son alisema ni hatua ya kuhakikisha wateja wanakuwa na wigo mkubwa kufurahia na kunufaika zaidi na huduma za mtandao huo bila kuwa na wasiwasi wa makato kila wanapotuma fedha mahali popote, na wakati wowote.

“Hii ni fursa nyingine ya kuongeza tabasamu na furaha kwa wateja wetu wa Halopesa inayoendana na hali ya uchumi kuondokana na usumbufu wanapotuma fedha. Sasa wataokoa makato ya miamala na kuzitumia fedha hizo kadiri wapendavyo,” alisema Son.

Licha ya kuondoa gharama za kutuma fedha kutoka Halopesa kwenda Halopesa, mkurugenzi huyo alisema wateja watapata muda wa maongezi bure kila wanapoweka fedha kwa wakala.

Alisema kila mteja atakayeweka kuanzia Sh1,000 kwa wakala atapata muda wa maongezi wa bure huku wakiendelea kunufaika kwa namna mbalimbali kila wanapotumia huduma hizo.

Kuzinduliwa kwa kampeni hiyo ni mwendelezo wa azma ya kuboresha huduma za fedha kwa njia ya mtandao kwa wananchi wenye vipato tofauti.

Licha ya kuondoa gharama za miamala kwa wateja wanaotuma fedha kutoka Halotel kwenda Halotel, kampuni hiyo imepunguza gharama za kutuma fedha kwenda mitandao mingine.

Advertisement