Uwekezaji Total sasa Sh460 bil

Tuesday May 14 2019

 

By Bakari Kiango, Mwananchi

Dar. Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameipongeza kampuni ya Total Tanzania kwa kuwekeza nchini mtaji wa Dola 200 milioni za Marekani (Sh460 bilioni) ndani ya miaka mitatu.

Pia amesifu ubunifu uliofanywa na kampuni hiyo wa kuwekeza zaidi ya Sh200 milioni kusaidia wajasiriamali kupitia mpango wa The African Start Upper Challenge.

Mpango huo ni shindano lililoandaliwa na Total ukiwa na lengo la kuwawezesha kimitaji wajasiriamali wadogo wenye mawazo mazuri ya biashara yatakayosaidia Taifa na jamii kuleta maendeleo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na ofisi ya Waziri Mkuu, Majaliwa alisema hayo wiki iliyopita wakati wa sherehe za kutimiza miaka 50 ya Total nchini, zilizofanyika Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Waziri wa Nishati, Dk Medard Kalemani, mabalozi, Rais wa Total Afrika na wafanyabiashara mbalimbali.

“Nimearifiwa kuwa tayari Watanzania sita wamenufaika na mpango huo kwa kupatiwa zaidi ya Sh25 milioni za kuanzisha shughuli mbalimbali za ujasiriamali,” amenukuliwa waziri mkuu.

Katika shindano la The African Start Upper Challenge la msimu wa pili, Doreen Peter Noni aliibuka kidedea na kujinyakulia Sh30 milioni, Sai Michael Sh20 milioni na Prince Tilya Sh15 milioni.

Naye Rais wa Total Afrika (masoko na huduma), Stanslas Mittelman alisema kampuni hiyo ilianzishwa mwaka 1969 na wamekuwa wakiamini uimara wa uhusiano wao na Serikali unatokana na uvumilivu na uaminifu wao kwa jamii.

Mittelman alisema uwekezaji wanaoufanya ni sehemu ya ukuaji wao. Pia, ni njia yao ya kushiriki kuchangia azma ya Serikali ya ukuzaji wa viwanda ili kuelekea Tanzania ya Viwanda.

“Tumeitikia wito wa Rais Magufuli wa kuongeza uwekezaji nchini,” alisema.

Advertisement