Vodacom yasaidia watoto wa mahitaji maalum

Wednesday March 6 2019

 

By Asna Kaniki, Mwananchi [email protected]

Mkuranga. Kampuni ya Vodacom Tanzania imetoa vifaa mbalimbali katika kituo cha watoto wenye uhitaji maalum ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya siku ya mwanamke duniani.

Vifaa hivyo vyenye thamani ya zaidi ya Sh 9 milioni vimetolewa leo katika kituo cha Mwanangu Special kilichopo kata ya Vikindu mkoani Pwani.

Akizumngumza wakati wa kukabidhi vivaa hivyo, meneja mawasiliano na matukio wa kampuni hiyo, Christina Murimi amesema msaada huo unalenga kusaidia watoto hao wenye matatizo mbalimbali kielimu ili waweze kutimiza ndoto zao.

“Tunawapongeza wazazi pamoja na walimu kwa kusaidia watoto hawa, lakini pia ni ujasiri walioutumia kuweka wazi watoto wao, tunaahidi tutaendelea kushirikiana nanyi,”amesema.

Mkuu wa wilaya ya Mkuranga, Filberto Sanga amewataka wazazi kutowaficha watoto wenye ulemavu na badala yake wawapeleke katika vituo vya watoto wenye uhitaji maalum ili wapatiwe huduma.

“Mtoto yeyote anayekuja ni zawadi hivyo tunavyowafungia kwa kuogopa kuchekwa ni kuwanyima haki zao za msingi, kwani huwezi jua anaweza akapona na akawa kiongozi mkubwa,” amesema Sanga.

Kwa upande wake, mkurugenzi wa kituo cha Mwanangu  Special Day Care, Walter Miya amesema ameamua kuanzisha kituo hicho ili watoto hao waweze kupata haki sawa na watoto wengine.

Amesema kutokana na mtazamo w jamii, watoto wenye ulemavu wa viungo au mtindio wa ubongo ni mzigo hivyo kutengwa na kuonekana hawana thamani.

“Watoto wenye ulemavu wa viungo na hata wa akili uwezekano wa kupona upo na wanaweza kuwa na mchango mkubwa katika jamii hivyo tusiwatenge wala kuwaficha tunakosea,” ameongeza.

Vodacom wametoa vifaa mbalimbali vikiwamo magongo ya kutembelea na kusimamia, mashine za kupima uzito pamoja na vitanda vya watoto wenye ulemavu.

 

Advertisement