Wakulima Ruvuma waomba viwanda zaidi

Baada ya Rais John Magufuli kuzindua kiwanda cha kukoboa na kusaga mahindi, wananchi mkoani Ruvuma wamesema kitaongeza uhakika wa soko la mavuno yao.

Ruvuma ni miongoni mwa mikoa inayolima mahindi kwa kiasi kikubwa hivyo kitendo cha Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kujenga kiwanda hicho kilichozinduliwa Aprili 8 na Dk Magufuli ni fursa inayotoa matumaini kwa wananchi wengi mkoani hapa.

Baada ya uzinduzi wa kiwanda hicho kilichogharimu Sh414.77 milioni, kikimilikiwa na kikosi cha JKT Mlale, wananchi wamepata matumaini mapya ya kuboresha kilimo na ufugaji pia.

Vene Mbunda mkazi wa Magagula wilayani Songea anasema kujengwa kwa kiwanda hicho kutainua uzalishaji wa mahidi kwani wananchi wana uhakika wa soko.

“Tulikuwa na wakati mgumu Serikali ilipokuwa inapiga marufuku usafirishaji wa mahindi nje ya nchi kwani walanguzi wa ndani hawalipi bei nzuri hivyo mkulima alikuwa ananyonywa,” amesema Vene.

Lakini uwepo wa kiwanda hicho ambcho ndicho kikubwa zaidi nchini, Vene anaamini kitajali masilahi ya wakulima na kutoa bei itakayowalipa ili waendelee kuimarisha kilimo.

Anasema kutokana na mabadiliko haya, bila shaka wenye uwezo wa kuongeza mashamba watafanya hivyo na watalima kisasa ili mahindi yao yakidhi vigezo vya kununuliwa na kiwanda hicho.

Kwa upande wake, Mwanahija Omary anasema mabadiliko ya maagizo ya Serikali kuhusu kusafirisha mahindi nchi jirani kama vile Rwanda, Msumbiji, Sudani Kusini na kwingineko huwa yanabadilika kila mara lakini ujenzi wa viwanda vya kudumu kama hiki cha kikosi cha Jeshi Mlale ni suluhu ya kudumu.

“Awali wakulima walikuwa wanapata taabu ya masoko ambapo mahindi yalishuka bei na kuwafanya waishi maisha magumu kutokana na kushindwa kumudu gharama za maisha na uzalishaji. Pembejeo walinunua kwa bei ya juu na mazao yao yalilanguliwa kwa bei ya chini,” anasema Mwanahija.

Endapo viwanda vingine vitafunguliwa maeneo mengi zaidi, anasema wakulima watapata fursa ya kukuza kipato hivyo kupambana na umasikini kwa kiasi kikubwa.

“Endapo kila zao litapata soko la uhakika, si ajabu wakulima nao wakaanza kumiliki viwanda vidogo licha ya kutoa malighafi hivyo kushiriki kikamilifu kwenye uchumi wa viwanda unaosisitizwa na Serikali,” amesema.

walikua wakiuza kwa walangiuzi kwa bei ya kutupa hivyo kufunguliwa kwa kiwanda kutachochea wakulima kuuza mahindi yao kwa bei nzuri zaidi Mwanahija.

Kwenye uzinduzi, mkuu wa Kikosi cha Jeshi Mlale, Meja Absoloom Shausi alisema ujenzi ulianza mwaka 2016 lakini kukoboa na kusaga mahindi wlaianza Januari mwaka jana.

Kuhusu uwezo, alisema wanaweza kukoboa na kusaga tani 440 za mahindi huku unga ukiuzwa jeshini na pumba zikiuzwa kwa wananchi kwa ajili ya chakula cha mifugo.

Rais Magufuli alizindua kiwanda hicho chenye uwezo wa kuzalisha tani 440 za unga na pumba tani 308 akiwa kwenye ziara kuizungukia mikoa ya kusini.

Kwenye ziara hiyo, alizindua miradi ya maendeleo ikiwamo barabara ya lami kutoka Mbinga kwenda Mbambabay.