Wananchi walia, chondechonde wafanyabiashara

Wachuuzi wakipanga jana samaki eneo la Dara wakisubiri wateja wanaofanya maandalizi ya mfungo wa Ramadhani. Picha na Muhammed Khamis

Muktasari:

Mmoja wa wafanyabiashara wa soko la Mwanakwerekwe, Rajab Ally alisema wakulima wengi au wanaoleta bidhaa hizo kutoka Tanzania bara ni chanzo cha bei kupanda.

Unguja. Baadhi ya wananchi visiwani hapa wamewataka wafanyabiashara kutotumia mwezi wa Ramadhani kupandisha bei ya bidhaa.

Wakizungza na gazeti hili katika maeneo tofauti jana, wananchi hao walisema imekuwa kawaida ifikapo Ramadhani bidhaa nyingi hupanda na kusababisha hali ngumu kwa watu.

Ramadhan Abdallah alisema wafanyabishara huutunia mwezi huu kukomoa wafungaji huku wakisahau ni wa kuomba msamaha na kuzidisha ibada.

“Kama bidhaa inauzwa sokoni hivi sasa kwa Sh5,000 ikianza Ramadhani bidhaa hiyo itauzwa zaidi ya hapo,” alisema Abdallah.

Naye Mayasa Kassim aliomba Serikali kupitia mamlaka zake kuhakikisha wanafanya ukaguzi kubaini wafanyabiashara wenye tabia ya kupandisha bei za bidhaa kipindi hiki ili wachukuliwe hatua. Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara walisema hawana nia ya kuongeza bei na wangetamani kuuza bei ya chini zaidi ila haiwezekani.

Mmoja wa wafanyabiashara wa soko la Mwanakwerekwe, Rajab Ally alisema wakulima wengi au wanaoleta bidhaa hizo kutoka Tanzania bara ni chanzo cha bei kupanda.

“Kwa mfano mkulima alikuwa aniuzia nazi moja kwa Sh300 ikifika tu Ramadhani ataniuzia nazi ileile kwa Sh600 sasa lazima na mimi nipandishe bei,” alisema.