Wasafiri Fastjet kusaidiwa

Dar es Salaam. Siku moja baada ya Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kutangaza kusitisha kuruka kwa ndege za Fastjet, Baraza la Utetezi wa Wasafiri wa Anga (TCAACCC) limewahakikishia abiria kupata haki zao.

Katibu mtendaji wa baraza hilo, Deborah Mligo alisema wanachokifanya ni kuhakikisha kila anayestahili, anapata haki yake tena kwa wakati.

“Tangu jana abiria wameanza kurejeshewa nauli zao. Yeyote aliyekata tiketi ya Fastjet afuate utaratibu kuhakikisha anarudishiwa nauli yake,” alisema.

Baraza hilo limeingia kazini kuhakikisha kila abiria anapata haki yake wakati shirika hilo likiendelea kuweka mambo yake sawa ili iwapo litaweza, linusurike kupoteza leseni ya biashara.

TCAA imeipa Fastjet notisi ya siku 28 kuthibitisha uwezo wake wa kujiendesha na kutoa huduma za uhakika kwa abiria.

Baada ya kauli ya mamlaka hiyo, Fastjet ilitangaza kurudisha nauli za abiria na wadau wengine kuanzia Desemba 20, lakini Deborah alisema kwa usimamizi wa baraza baadhi ya abiria wameanza kulipwa.

Bila kujali abiria alilipia nauli yake kwa njia ipi, Deborah alisema anachotakiwa kufanya ni kwenda ofisi za Fastjet au wakala wake arudishiwe nauli yake.

Kwa watakaopata usumbufu wowote, alisema wanaweza kuwasiliana na baraza hilo kwa namba 0719 100 600 au kutuma baruapepe kwenda info@tcaa_ccc.go.tz.

“Tiketi yako ndiyo mkataba wako muhimu. Ili ulipwe nauli yako ni lazima uwe nayo,” alisema katibu huyo.