Breaking News

Mataifa yaahidi kuimwagia misaada lukuki Sudan Kusini

Monday July 11 2011

JUBA, Sudan Kusini
MATAIFA mbalimbali duniani yameahidi kuisadia nchi mpya ya Sudan Kusini baada ya kujitenga na kuwa taifa huru.
Misaada pia itawezesha taifa hilo jipya kuanzisha mfumo imara wa kisiasa pamoja na kuwa na maendeleo lukuki nchini humo.

Rais wa China, Hu Jintao jana ametoa pongezi lukuki mjini Beijing kwa nchi ya Sudan Kusini kuwa huru na ameahidi kushirikiana na nchi hiyo pamoja na kuingia mkataba nayo katika masuala ya usambazaji wa mafuta.

China ambayo ni mnunuaji wa mafuta ya Sudan na alikuwa anahakikisha kuwa kutengana kwa sehemu hizo mbili hakutaleta madhara katika ununuaji wa mafuta katika nchi yake.

Katika hotuba yake ya kila wiki kupitia kanda ya video, Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel jana alisema kuwa baada ya Sudan Kusini kujitenga na kuwa taifa jipya, nchi yake itaisaidia nchi hiyo ili iwe na mfumo bora wa kisiasa.

“Sasa ni muhimu kuiunga mkono Sudan Kusini, kuelekea utulivu utakaowaletea watu wa eneo hilo amani, usalama na maendeleo ya kiuchumi,” alisema Merkel.

Hata hivyo, kuanzia leo Jumatatu, Kansela Merkel anatarajia kulitembelea bara la Afrika kwa mara ya pili aikiwa ni kiongozi wa serikali, kuanzia leo hadi siku ya Alhamisi.
Kiongozi huyo anatarajia kuzitembelea Kenya, Angola na Nigeria.

Advertisement

 Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Ban Ki-moon, alisema umoja huo umeunda kikosi kipya kwa ajili ya Sudan Kusini cha kusaidia kuimarisha amani pamoja na kutoa misaada mbalimbali ya kimaendeleo nchini humo.
Pia alizisihi nchi za Sudan na Sudan Kusini kushirikiana.

Alisema nchi hizo ni kama ndugu hivyo licha ya kutengana, ushirikiano ni muhimu kwa ajili ya vizazi vijavyo.
 “Ni nafasi ya kuthibitisha tena ahadi ya kujenga uhusiano wa amani, wenye manufaa na kukabili hatima yao kama washirika - siyo washindani," alisema Ban Ki-moon.

Aliongeza kwamba, pande hizo mbili hazijafikia muafaka juu ya namna ya kugawana mafuta na mapigano yamezuka katika maeneo ya mpaka baina yao.

Nayo Marekani, kupitia balozi wake katika Umoja wa Mataifa, Susan Rice alisema Marekani ipo bega kwa bega taifa hilo jipya na itahakikisha inashirikiana vizuri na nchi hiyo.

Kabla ya sherehe za uhuru huo, Ikulu ya Marekani ilimteua Rice kuongoza ujumbe wa nchi hiyo katika sherehe hizo za uhuru.

Katika sherehe hizo ambazo ziliungwa mkono na Rais wa Sudan, Omar al-Bashir ambapo aliuambia umati ulioudhuria sherehe za uhuru na viongozi wa kimataifa, kwamba Sudan imetimiza ahadi yake.

Alisema wengi hawakuamini kuwa Khartoum itaiacha Sudan Kusini yenye utajiri wa mafuta, ijitenge.

"Ni wakati wa Marekani nayo kutimiza ahadi yake, na iondoshe vikwazo dhidi ya Sudan,” alisema Rais Bashir.
Vikwazo hivo vinaleta shida kwa uchumi wa Sudan, ambayo sasa, baada ya Sudan Kusini kupata uhuru, pia imepoteza mafuta mengi.

Rais Bashir piya alitoa wito kuwepo uhusiano wa amani na Sudan Kusini, lakini alikiri kuwa usalama kwenye mpaka wa karibu kilomita elfu mbili baina yao, utakuwa changamoto kubwa.

Uhuru wa Sudan Kusini umetokana na mkataba wa amani wa mwaka 2005 uliomaliza mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyodumu kwa miaka mingi.

Sudan Kusini inakuwa taifa la 193 duniani, na kutambuliwa na Umoja wa Mataifa, na pia kuwa taifa la 54 barani Afrika.

Naye Salva Kiir Mayardit ambaye amekubaliwa na wananchi wa taifa hilo kuingoza nchi hiyo alitoa kipaumbele cha kuboresha miundombinu nchini humo ikiwa ni pamoja na ushirikiano.
REUTERS

Advertisement