Breaking News

Museveni aitisha kikao cha dharura kujadili Uchumi

Friday August 5 2011

KAMPALA,Uganda,BBC
RAIS Yoweri Museveni amelazimika kuitisha  kikao cha dharura cha mawaziri kujadili jinsi ya kukabili hali mbaya ya uchumi nchini humo.

Baraza hilo la mawaziri linakutana katika kipindi ambacho viongozi wa upinzani wamekuwa wakilalamikia kupanda kwa gharama za maisha.

Bidhaa muhimu kama vile sukari zimeanza kukosekana madukani hali ambayo inawaathiri watu wenye kipato cha chini nchini humo.

Mwandishi wa BBC mjini Kampala alisema bei ya sukari imepanda kiasi kwamba kile kiasi kilichoko aidha kinafichwa ama kuniauzwa bei kali ambayo sio ile ya kawaida.

katika maduka makubwa watu hawakubaliwi kununua zaidi ya kilo moja.

Hali hii inatishia uchumi wa taifa ambao kwa sasa kwa mujibu wa gavana wa benki kuu ya taifa kiwango cha ukuaji wa uchumi wa Uganda kitadidimia kwa asilimia 5 kutokana na kiwango kikubwa cha mfumuko wa bei za bidhaa.
Mfumuko wa bei unakaribia asilimia 20, kiwango kikubwa zaidi kwa kipindi cha miaka 10.

Advertisement

Pia kiwango cha ubadilishanaji wa pesa za Uganda kwa dola kumepanda kiasi kuwa dola 1 inanunua shilling za Uganda 2,634.

Msemaji wa serikali na waziri wa habari Mary Okurut alisema kikao hicho maalum cha mawaziri kitajadili mikakati ya kukabili hali hii ya uchumi.

Kuhusu kutoweka kwa sukari madukani, waziri Okurut amesema kuwa serikali imeomba ruhusa kutoka jumuiya ya Afrika mashariki ikubaliwe kuagizia sukari kutoka nje ya ukanda huu.

Uganda ina viwanda vitatu vinavyozalisha sukari, lakini ni kimoja tu kwa sasa kinachofanya kazi.
Viwili vilivyosalia, kimoja kimefungwa kwa sababu mitambo yake inafanyiwa ukarabati ilhali kingine kwa kuwa hakipati miwa inayotosheleza uzalishaji

Wakati huo huo Shirika  la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limetahadharisha kuwa Uganda pia inaelekea kukumbwa na baa la njaa ambalo linashuhudiwa hivi sasa katika nchi za Pembe ya Afrika.

Msemaji wa shirika la FAO alisema kuwa, kutokana na kuelekea kumalizika akiba ya chakula nchini Uganda, usalama wa chakula kwa taifa hilo upo hatarini na huenda wananchi wake wakapatwa na yale yanayoshuhudiwa hivi sasa katika nchi za Somalia, Kenya, Ethiopia na Djibouti.

Advertisement