Sekta ya mifugo inahitaji mipango kuongeza mchango pato la Taifa

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Dk Joel Bendera, (wapili kushoto) na viongozi wa Mbulu wakiwa wameshika vyuma kwa ajili ya kupiga chapa mifugo katika hafla ya uzinduzi wa usajili, utambuzi na upigaji chapa wa mifugo katika Kijiji cha Hayloto wilayani Mbulu, jana. Kushoto ni Mkuu wa wilaya ya hiyo, Chelestino Mofuga na wa tatu kushoto ni mkurugenzi wa mji huo, Anna Mbogo. Picha na Joseph Lyimo

Miaka ya nyuma kidogo, Tanzania iliamini katika sera ya kilimo na kujitegemea. Zilikuwa zama za Azimio la Arusha lililokuwa linahamasisha na kuutetea ujamaa.

Inawezekana ndio msingi uliojengwa mpaka hivi leo Tanzania inajitegemea kwa chakula. Inalima na kuzalisha kwa zaidi ya asilimia 100 huku ikiwa miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya mifugo.

Takwimu zilizopo zinaonyesha Tanzania ina zaidi ya ng’ombe milioni 30.5, mbuzi milioni 18.8 na kondoo milioni 5.3 Vilevile ina kuku wa asili milioni 38.2, kuku wa kisasa milioni36.6. Bado, kuna nguruwe milioni 1.9 na punda 595,160.

Pamoja na idadi hiyo, wadau wanafahamu ni lita bilioni 2.4 za maziwa zinazalishwa kila mwaka, kiasi kinachomruhusu kila Mtanzaniakunywa wastani wa lita 47 badala ya lita 200 kwa mwaka zinazopendekezwa na Shirika la Chakula na Kilimo Duniani (FAO).

Licha ya kuwa na faida nyinginezo kama vile uzalishaji wa nyama, kwato, ngozi na mbolea, ufugaji nchini hauchangii vya kutosha kwenye uchumi na ajira kutokana na kutokuwa na mipango mizuri inayowahusisha wafugaji wadogo ambao ndio wengi zaidi.

Mwanasheria wa Shirika la Ping’os Forum, Emmanuel Salinge anasema Wizara ya Mifugo na Uvuvi imejielekeza kwa wafugaji wenye ranchi na kuwasahau wafugaji wadogo.

“Mipango ya wizara haionyeshi kushughulika na utatuzi wa matatizo ya mfugaji mmoja mmoja. Ziara nyingi ni kwenda kwenye ranchi takwimu zinaonyesha mifugo mingi ipo kwa wafugaji wadogo ambao kama wangeboreshewa mazingira mchango wa sekta hiyo ungeongezeka mara mbili ya sasa,” anasema.

Taarifa za Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) zinaonyesha kwa mwaka 2016, mifugo ilikua kwa asilimia 2.6 na kuchangia asilimia 6.9 kwenye pato la Taifa na mwaka 2017 ilikua kwa asilimia 2.8 na kuchangia asilimia 7.7.

Ardhi

Ufugaji ni uwekezaji wenye fursa ya kuchangia pato la Taifa, kuongeza ajira na kuondoa umasikini lakini kwa muda mrefu umekuwa wa kuhamahama hivyo kukosa mashiko na kutolipa.

Mara nyingi migororo ya ardhi imesababisha mapigano yaliyopoteza ama maisha ya binadamu au mifugo huku ekari za mazao zikiharibiwa. Hili ni jukumu la Serikali, wazee wa mila na wadau wengine wa ardhi kuweka mkakati wa kumaliza migogoro hii ili kuimarisha ufugaji na kuongeza mchango wake.

Si ajira na kuchangia pato la Taifa pekee, ufugaji ni chanzo cha uhakika cha chakula, lishe ya uhakika na malighafi za viwanda. Kuimarisha sekta ya mifugo kunahitaji usimamizi makini wa ardhi kwa kutenga maeneo ya malisho, vyanzo vya maji, huduma za utafiti na mafunzo.

Katibu wa chama cha wafugaji Tanzania, Magembe Makoye anasema ranchi 14 zilizopo zina mifugo isiyozidi 300,000 kati ya mamilioni iliyopo nchini.

“Nyingine zimekodishwa kwa watu wanaolipa fedha kidogo serikalini huku wakiingiza wafugaji kutoka nje kwa gharama kubwa. Tumepiga kelele tupewe sisi hawasikii na kila siku wanaelekeza nguvu huko,” anabainisha Makoye.

Kingine kinachochelewesha maendeleo ya sekta hiyo, Makoye anasema ni mwingiliano uliopo serikalini ambako maofisa mifugo wanafanya kazi chini ya mkurugenzi wa halmashauri ingawa wanawajibika kwa wizara ya mifugo.

“Kuna minada mingi ambayo inaingiza mabilioni ya fedha zinazoishia kulipana posho na hakuna kinachorudishwa kendeleza ufugaji. Hakuna anayewasemea wafugaji maana wizara haiko karibu nao,” anadai katibu huyo.

Kwenye hotuba ya bajeti ya mwaka huu wa fedha, Serikali ilisema kuna utoroshaji mkubwa wa rasilimali na mazao ya mifugo unaochangiwa na biashara za magendo hivyo Taifa linapoteza zaidi ya Sh263.95 bilioni kwa mwaka jambo wadau wanasema linasababishwa na kutokuwapo kwa uhusiano wa moja kwa moja kati ya wizara wafugaji.

Uwekezaji

Mjumbe wa kamati tendaji ya chama cha wafugaji kanda ya ziwa, Menasi Kiruri anasema kama kungekuwa na unaoeleweka, wafugaji wana uwezo wa kuanzisha benki yao.

“Kuna takriban wafugaji milioni sita nchini, endapo kila mmoja atachanga Sh200,000 zitapatikana zaidi ya Sh1.2 trilioni ambazo zinatosha kuanzisha benki itakayotoa mikopo kwa wafugaji kuanzisha viwanda,” anasema Kiruri.