Kuna Mtanzania mmoja miongoni mwa vijana 30 anaowahusudu Bill Gates Afrika

Rais John Magufuli akipeana mkono na Mwenyekiti wa  Taasisi ya Bill and Melinda Gates Foundation, Bill Gates alipokuwa akiagana naye baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao Ikulu jijini Dar es salaam jana. Kulia ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto,Ummy Mwalimu na kushoto ni Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dk Charles Tizeba.  Picha na Ikulu

Muktasari:

  • Watu wengi hufurahi wanapokutana na watu wanaowapenda kutokana na upekee wanaoufanya kwenye shughuli zao za kila siku. Mara nyingi, imezoeleka, watu wa chini huwapenda walio juu kimaisha. Tofauti na mtazamo huo, tajiri namba moja duniani, Bill Gates amesema anachokipenda kila anapotembelea Afrika na kuwataka watu wengine kuzuru Afrika kujionea anayoyaona.

Kwa sasa, dunia ina zaidi ya watu bilioni 7.63 na kati yao, bilioni 1.2 wananishi Afrika. Zaidi ya watu bilioni sita wanaishi kwenye mabara mengine ingawa hupata fursa ya kuja kutembea kwa sababu mbalimbali.

Unaweza ukawa unawafahamu watu wengi maarufu kutokana na shughuli zao wanazozifanya. Kuna wanasiasa, watetezi wa haki za binadamu, waandishi wa habari, wafanyabiashara, wanamuziki na wanamichezo au wajasiriamali.

Kwenye orodha ya watu wanaofahamika zaidi ni Bill Gates, tajiri namba moja duniani kote. Ndio, majarida na taasisi mbalimbali zimemthibitisha kuwa na ukwasi mrefu zaidi kukizidi kiumbe chochote kinachoishi kwa sasa.

Utajiri wake unatokana na kuanzisha na kumiliki kampuni ya Microsoft inayotoa huduma na bidhaa mbalimbali za Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama). Kutokana na kiasi kikubwa cha fedha, Gates amekuwa akitoa misaada mbalimbali ya kijamii za Serikali hasa za ulimwengu wa tatu kupitia taasisi yake ijulikanayo kama Melinda and Bill Gates Foundation.

Gates ni miongoni mwa watu wanaopenda kuitembelea Afrika. Amefanya hivyo mara kadhaa. Hivi karibuni alihudhuria harusi ya binti wa tajiri namba moja Afrika, Mnigeria Aliko Dangote ambako watu wengine maarufu walialikwa.

Agosti mwaka jana, tajiri huyo alitembelea Tanzania kuja kukagua miradi inayotekelezwa na taasisi yake. Vilevile, alikuja kuona vipaumbele vya Serikali na kufahamu namna anavyoweza kusaidia kuvifanikisha.

Kwenye ziara hiyo, tajiri huyo aliahidi kutoa Dola 15 milioni za Marekani ili kuboresha mfumo wa afya wa kidijitali kutunza takwimu za wagonjwa, wagonjwa na utafiti unaofanywa kwenye sekta hiyo.

Pamoja na maeneo mengine aliyotembelea kipindi hicho ni pamoja na kukutana na Rais John Magufuli Ikulu jijini Dar es Salaam pamoja na viongozi wengine waandamizi wa Serikali.

Kati ya mwaka 2001 na 2016, taarifa zinaonyesha taasisi ya tajiri huyo Mmarekani imewekeza zaidi ya Dola 9 bilioni na inatarajia kuwekeza Dola 5 bilioni mpaka mwaka 20121.

Afrika

Kwa zaidi ya miongo miwili iliyopita, Gates amekuwa akifanya ziara nyingi barani Afrika. Iwe kwa ajili ya mapumziko au kukutana na wadau watunga sera au kuhudhuria mikutano ya wadau wa maendeleo, hutenga nafasi ya kukutana na vijana wenye mawazo mbadala.

Kutokana na uzoefu alioupata kwene safari zake hizo, Gates anawaalika watu wengine wakubwa duniani kuja Afrika na kuona hazina kubwa ya ubunifu iliyopo. Mwaliko huo huwa anaotua hadharani, iwe kupitia vyombo vya habari au kwenye mikutano na makungamano tofauti anayohudhuria.

Kwenye ukurasa wake wa Twitter wiki hii ameendeleza ari hiyo kwa kuwakumbusha zaidi ya watu milioni 46 wanaoifuatilia kuhusu suala hilo.

“Nimekuwa nikitembelea nchi za Afrika kwa zaidi ya miongo miwili iliyopita. Natamani wengine wangefanya hivyo pia ili kujionea ninachokishuhudia mara nyingi: bara changa lenye ubunifu na matumaini,” ameandika tajiri huyo.

Ujumbe huo wa Bill Gates ulisindikizwa na orodha ya wabunifu, wavumbuzi, wajasiriamali na watafiti vijana 30 wa Afrika iliyoandaliwa na Jarida la Quartz Africa.

Tangu mwaka 2015, jarida hilo limekuwa linaloripoti taarifa za uvumbuzi na ujasiriamali unaofanywa Afrika na Waafrika wenyewe kutatua changamoto zao. Huwatambua pia Waafrika walio nje ya bara lakini wakiwa na mchango mkubwa kwa Afrika.

Gates ame-tweet toleo la nne la orodha ya vijana hao 30 mwaka huu akitambua mchango wao kiuchumi na kijamii kutokana na shughuli zao wanazozifanya maeneo tofauti.

Licha ya itofauti wa taaluma na shughuli zao, vijana hao huunganishwa na kimoja tu, nia yao ya dhati ya kufanya mabadiliko kwenye jamii au nchi zao hata bara zima kwa ujumla.

“Tunaamini uvumbuzi si kwenye sayansi na teknolojia pekee bali ubunifu wa ziada unaorahisisha maisha kwa kuondoa changamoto zilizopo. Tunatambua suluhu inayotolewa kwenye kilimo, kukabili maradhi hata mapigo ya muziki wenye mahadhi tofauti,” anasema Yinka Adegoke, mhariri wa Quartz Africa.

Mhariri huyo anasema kuna uhusiano kati ya kasi kubwa ya ongezeko la watu Afrika na ukosefu wa ajira hasa kwa vijana, ongezeko la maambukizi ya magonjwa tofauti na mabadiliko ya tabianchi kati ya athari nyingi zinazojitokeza.

Kukabiliana na changamoto hizo, Adegoke anasema kunahitaji utulivukatika kufikiri, viongozi makini na ubunifu wa kuzishughulikia. “Wanawake na wanaume hawa wanathibitisha umuhimu wa kutafuta suluhu za matatizo ya Afrika itatafutwa na Waafrika wenyewe,” anasema mhariri huyo.

Tanzania

Tangu kuanza kutolewa kwa orodha hiyo, kila mwaka, Mtanzania mmoja huwa hakosekani. Mwaka 2015 wakati taarifa hiyo inaandaliwa, ilimtambua Profesa Julie Makani, mtafiti wa damu na magonjwa yake wa Chuo Kikuu cha Afya Muhimbili (Muhas).

Mwaka uliofuata (2016) ikawa zamu ya Edwin Bruno, mwanzilishi wa kampuni ya Smart Codes inayohusika na ununuzi wa matangazo na kuziwezesha kampuni nyingine kuonekana kwenye mitandao ya kijamii, tovuti na intaneti kwa bei nafuu.

Mwaka 2015, Edwin na kampuni yake walishinda tuzo na ubunifu wao kutambuliwa kimataifa baada ya kubuni App ya M-Paper inayomuwezesha mtu kusoma magazeti ya kila siku mtandaoni kwa kulipia nusu ya bei kwa kutumia kompyuta au simu ya mkononi.

Mwaka jana, jarida hilo lilimtambua Lilian Makoi mwanzilishi wa kampuni ya Edge Point iliyobuni mfumo wa kidijitali kufanikisha kufikisha huduma za bima kwa wananchi wa kipato cha chini.

Na mwaka huu, kwenye orodha hiyo iliyopewa kipaumbele na Bill Gates yumo Profesa Fredros Okumu, mkurugenzi wa sayansi wa Taasisi ya Utafiti Ifakara.

Malaria yambeba

Kutoka Ifakara alikokulia, Profesa Okumu ni mhanga wa malaria ambaye ameamua kutafuta suluhu si itakayomsaidia yeye pekee bali dunia nzima inayoangamizwa na mdudu huyo mdogo.

Kufanikisha lengo hilo, anafanya utafiti kujua ni kwa namna gani mbu hueneza malaria tangu anapozaliwa. Katika jitihada hizo, anaangalia uwezekano wa kumfuatilia na kumdhibiti mbu asisababishe malaria hivyo kuuondoa ugonjwa huo duniani.

Huko Ifakara (chuoni), profesa huyo anafuatilia tabia za mbu kuanzia anavyonusa hivyo kutofautisha harufu ya mtu mmoja na mwingine ndani ya nyumba au popote walipo zaidi ya mtu mmoja mpaka jinsi wanavyopandana na kuzaana.

Inaelezwa, mbu hupandana kwa kucheza pamoja wakirukaruka sehemu moja, mwaka mmoja mpaka mwingine. Hufanya hivyo sehemu moja.

Sh1.4 bilioni

Kutokana na juhudi zake, Profesa Fredros Okumu ni miongoni mwa wanasayansi na watafiti 41 kutoka nchi 16 duniani ambao wamechaguliwa kufanya utafiti wa kitabibu dhidi ya magonjwa yanayosumbua wananchi wengi.

Uteuzi huo umefanywa na Taasisi ya Afya ya Howard Hughes (HHMI) ikishirikiana na Bill & Melinda Gates, Calouste Gulbenkian na Wellcome Trust zilizotoa kiasi cha Dola 26.7 milioni za Marekani kwa kila mmoja. Katika fedha hizo, kila mtafiti atapokea Dola 650,000 (zaidi ya Sh1.4 bilioni) ndani ya miaka mitano.

Mradi wa Profesa Okumu unajikita kutafuta suluhu ya kudumu ya kukabiliana na mbu waenezao malaria, ugonjwa unaoua watu wengi Tanzania na duniani kwa ujumla.

“Hawa ni watafiti watakaosaidia kusukuma gurudumu la utafiti wa kibayolojia mbele. Tunawasaidia kufanikisha ndoto zao kwa kushirikiana na wahisani wetu,” David Clapham, makamu wa rais na mwanasayansi mkuu wa taasisi ya HHMI alipokuwa anatangaza orodha ya washindi wa fedha hizo kati ya waombaji 1,400 waliojitokeza.

Profesa Okumu alipata nafasi ya kuwa miongoni mwa watafiti hao wachache duniani kwa mwaka 2017 katika shindano lililowashirikisha wanasayansi wanafanyakazi na taasisi ya utafiti, chuo kikuu, chuo kikuu cha tiba au shirika lisilotengeneza faida na ambaye amekuwa akifanya utafiti kwa miaka isiyozidi saba.

Prosefa Okumu

Profesa Fredros Okumu ni mkurugenzi wa sayansi katika Taasisi ya Utafiti Ifakara (IHI), mhitimu wa shahada ya afya ya jamii kutoka Chuo Kikuu cha Moi, Kenya. Licha ya shahada ya kwanza, ni mhitimu wa shahada ya uvamivu kutoka Chuo Kikuu cha London, Uingereza.

Licha ya utafiti wa magonjwa, ni mkufunzi wa magonjwa ya afya ya jamii Chuo Kikuu cha Witwatersrand, Afrika Kusini, mtafiti mwalikwa wa Chuo Kikuu cha Minas Gerais, Brazil na mtafiti mwenza wa heshima wa Chuo Kikuu cha afya cha Glasgow cha Uingereza.

Mwaka 2016, Profesa Fredros alitajwa kuwa miongoni mwa watu 100 wanaofikiri zaidi (Top 100 Global Thinkers) na Jarida la Sera ya Mambo ya Nje la Marekani.

Profesa Okumu pia alitunukiwa tuzo ya mtafiti kijana mwaka 2009 na Chama cha Wataalamu wa Magonjwa ya Kitropiki cha Marekani.