Mnara wa Azimio la Arusha ‘umepoteza’ historia yake

Monday March 23 2015

 

By Moses Mashalla

Ukifika katikati ya Jiji la Arusha, utakutana na mnara wa kumbukumbu ya mahali ambako Azimio la Arusha liliasisiwa na kuzaliwa mnamo mwaka 1967 chini ya Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Unaweza kushangaa na kujiuliza kwamba watalii wanaofika kufanya ziara ya kuutembelea wanawezaje kupata taarifa sahihi?

Jibu ni kwamba, wakifika huishia kupiga picha bila kupata maelezo ya kina, kisha kuondoka.

Nini chanzo?

Sababu ya kuondoka bila historia ya mnara huo ni kuibwa kwa kibao chenye maelezo ya kumbukumbu za ujenzi wake.

Kibao hicho kilichotengenezwa kwa madini ya shaba kiliibiwa na watu wasiojulikana mwaka jana waliotokomea nacho kusikojulikana bila kukamatwa hadi sasa.

Meneja wa Bodi ya Utalii, Tawi la Arusha, Willy Lyimo anasema kuibwa kwa kibao hicho kumesababisha usumbufu mkubwa kwa watalii wanaofika kutembelea mnara huo.

Anasema baadhi ya watalii wanaofika hapo hushindwa kupata historia kamili ya mnara huo hata kupiga picha kwa kutoonekana kwa kibao kinachoelezea historia yake.

‘Hii ni ajabu sana, mnara wa kumbukumbu wa Azimio la Arusha unakosa kuwa na historia? Watalii wanapata tabu kupata taarifa za mnara huo kwamba ulijengwa lini na ulizinduliwa na nani au maana yake nini,” anasema Lyimo.

Mbali na watalii, Lyimo anabainisha kundi jingine linalopata usumbufu kwa kutokuwapo kibao cha maelezo kuhusu mnara huo kuibwa ni wanafunzi wa shule za msingi, sekondari na vyuo ambao hufika kujifunza historia ya mnara huo wenye kumbukumbu nzito ya Taifa la Tanzania ambao pia ni urithi wa vizazi vijavyo.

Hata hivyo, Lyimo anasisitiza kuwa Bodi ya Utalii tawi la Arusha inaendelea kusaka kibao hicho huku ikitafuta maneno yaliyoandikwa kwenye kibao hicho ili kutengeneza kibao kipya.

Anasema hivi karibuni walikwenda Wizara ya Maliasili na Utalii, Idara ya Mambo ya Kale, lakini hawakufanikiwa kupata kumbukumbu ya namna yoyote inayoelezea historia ya mnara huo.

Lyimo anasema mbali na kubisha hodi wizarani pia walifika katika Idara ya Makumbusho ya Taifa, mkoani Arusha iliyopo mkabala na mnara huo, lakini pia hawakufanikiwa kupata kumbukumbu ya aina yoyote.

“Tumeshahangaika huku na kule kutafuta maneno yaliyomo katika kibao hicho ili tutengeneze kingine kwa gharama yetu bila mafanikio,” anasema Lyimo.

Hata hivyo, Lyimo anasisitiza ya kwamba kwa sasa eneo lililoibwa kibao hicho kumewekwa tangazo la Mamlaka ya Maji Safi na Majitaka mkoani Arusha(Auwsa) baada ya kuwa wazi, hadi kitakapopatikana kibao kingine cha kuwekwa eneo hilo.

Mbali na kuweka tangazo hilo, mamlaka hiyo ya maji mkoani Arusha, pia imesaidia kuboresha mazingira yanayouzunguka mnara huo kwa kuweka uzio na kutengeneza bustani ya maua.

Polisi

Akizungumzia wizi wa kibao hicho, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Liberatus Sabas anasema hawajapokea taarifa rasmi kuhusu kuibwa kwa kibao hicho chenye madini ghali ya shaba. Anasema iwapo kuna taarifa kama hizo, ni vyema wahusika wakatoa taarifa polisi, ili wao waanze juhudi za kuwasaka na kuwakamata wanaohusika na wizi huo.

“Wao wametangaza kwamba kibao kimeibwa, hivyo ni vyema wakatoa taarifa kwa mamlaka husika ili sisi tuweze kuishughulikia hiyo taarifa,” anasema Sabas.

Mhifadhi Azimio la Arusha

Mhifadhi wa Makumbusho ya Azimio la Arusha, Constantine Nyamabondo anasema usimamizi wa mnara huo ulishaondolewa chini yao na kukabidhiwa kwa Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Kuhusu suala la kumbukumbu za mnara huo anasema zipo huku akitoa wito kwa mtu au taasisi yoyote inayozihitaji kufika katika ofisi zao.

“TTB kama wanataka historia ya maandishi na wanataka kutengeneza kibao kingine, sisi tupo tayari kushirikiana nao bila tatizo,” anasema Nyamabondo.

Jiji la Arusha

Meya wa Halmashauri ya Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo pamoja na mkurugenzi wa jiji hilo, kwa nyakati tofauti, walionyesha kushangangazwa na tukio hilo huku wakiahidi kulifuatilia kwa undani ili kubaini ukweli.

Wanaeleza kwamba kitendo cha uongozi wa jiji hilo kutokuwa na ofisa utamaduni kumechangia kushindwa kufuatilia masuala mbalimbali likiwamo la kibao cha historia ya Azimio la Arusha kuibwa.

Hata hivyo, Mashaka Ngwabi mkazi wa Arusha aliyeshiriki ujenzi wa mnara huo, anasema anazijua kumbukumbu zake na atashirikiana na mamlaka yoyote itakayohitaji maneno hayo.

Anasema kuwa baadhi ya maandishi katika kibao hicho kilichokuwa na uzito wa kilo 15 yalisomeka: ”Mnara huu wa kumbukumbu ya Azimio la Arusha Umezinduliwa na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere mwaka 1967.”

Advertisement