Lowassa, Mtoto wa tarishi anayetaka urais

Friday June 5 2015Mbunge wa Monduli Edward Lowassa

Mbunge wa Monduli Edward Lowassa 

By Mussa Juma

Monduli. Kwa akili za kawaida, huwezi kutabiri kwamba mtu fulani ambaye labda ameanza siasa zamani au hata ni mwanasiasa chipukizi, siku moja atafikia hatua ya kuutaka urais katika nchi yake. Historia zinaonyesha kuwa marais wengi wameibuka tu hivyo hivyo.

Miongoni mwa wanasiasa wenye historia za kustaajabisha ni Edward Lowassa, Waziri Mkuu wa zamani ambaye sasa ametangaza tena nia ya kusaka ridhaa ya CCM kuwania urais katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu.

Edward ni mtoto wa nne, katika familia ya marehemu Ngoyai Lowassa, ambaye alikuwa akifanya kazi ofisi ya serikali ya kikoloni ya wilaya ya Monduli kama tarishi akiwa pia mfugaji.

Alivyoondolewa machungaji

Mzee John Kimati Ngao, Mkazi wa Monduli Mjini anasema alimfahamu Edward tangu mwaka 1964, wakati huo akisoma shule ya kati ya Monduli (middle school).

Anasema shamba lake lilikuwa jirani na nyumbani kwa Mzee Ngoyai na Edward alikuwa akipita hapo kwenda kuchunga mifugo kila alipotoka shule.

Advertisement

Mzee Ngao anasema bahati nzuri Lowassa alifanikiwa kufaulu shule ya msingi, hivyo akapata nafasi ya kwenda kusoma Shule ya Sekondari Arusha.

“Kwa kuwa ilitokea tukazoeana sana akawa kama rafiki yangu. Sikupenda alipokuwa anakwenda kuchunga mara kwa mara bila kwenda shule hivyo, nilitoa fedha akaenda sekondari. Sikumbuki kwa mara ya kwanza ilikuwa ni shilingi ngapi lakini baadaye nilimpa kati ya Sh1,500 na Sh2,000,” anasema Mzee Ngao.

Mzee Ngao anasema alikuwa akimpa fedha Edward tangu wakati alipokuwa akisoma kidato cha kwanza hadi cha sita Shule ya Sekondari ya Milambo mkoani Tabora na alifanya hivyo kwa jinsi alivyokuwa akimpenda hasa kutokana na kujituma kwake.

“Ninaposikia leo anagombea urais najisikia vizuri, kwani ninamfahamu tangu utoto na naamini anaweza kuwa kiongozi mzuri tu akisaidiana na wenzake,” anasema.

Alipokuwa sekondari

Elibariki Kelele, mmoja wa watu waliosoma na Edward Lowassa, Monduli Middle School hivi sasa inajulikana kama Moringe Sekondari, anasema mwanasiasa huyo alianza uongozi akiwa shuleni hapo, akianzia uongozi wa bendi ya shule hiyo. Anasema alikuwa msafi sana na alipendwa sana.

“Alikuwa mchapakazi anapendwa na kila mtu, alikuwa anapenda sana kuzungumza Kiingereza na ndio sababu walimu wazungu wa kujitolea walikuwa wakimpenda sana,” anasema.

Anasema licha ya kupenda shule, Lowassa pia alipenda kwenda kuchunga mifugo na walikuwa wakienda naye machungani.

Mwalimu anasemaje?

Reuben Ole Kuney, mmoja wa wanafunzi wa kwanza kutoka wilaya ya Monduli, kupata elimu ya chuo kikuu, anasema alikuwa akimfundisha Lowassa kila alipotoka chuoni. “Alikuwa anapenda sana kujifunza, ingawa nilikuwa nampita kama miaka 12 hivi, alikuwa akinifuata nimfundishe masomo mbalimbali na binafsi nilitokea kumpenda sana,” anasema.

Anasema wakati wote wakiwa shuleni au machungani, Lowassa alikuwa ni mdadisi wa mambo.

“Wakati nasoma shahada ya elimu pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, tulitakiwa kuandika stadi za watu tunaowajua, yaani kuandika maisha yao na kumbukumbu zao, mimi niliandika juu ya Edward Lowassa na nilipata alama A.”

Anasema wakati wote Lowassa alikuwa anaonyesha kuwa anaweza kuja kuwa kiongozi, kwani alikuwa anapenda kujifunza pamoja na kufuatilia mambo mbalimbali yakiwamo ya siasa.

“Wakati Edward akiwa chuo kikuu, alikuwa pamoja na Rais Jakaya Kikwete na John Chilligati, hawa wote baadaye walijishughulisha na mambo ya siasa.

“Edward amekuwa na mitazamo ya mabadiliko wakati wote. Haya matatizo ya ajira na mambo mengine tangu wakati huo, alikuwa akizungumzia,” anasema.

Kuney, ambaye ameshika nafasi kadhaa serikalini, ikiwamo ukuu wa wilaya kabla ya kustaafu, anaamini bado safari ya Lowassa kisiasa inakwenda vizuri na ipo siku Mungu atatimiza ndoto zake.

Hasimu wake kisiasa

Lapilali ole Molloiment aliyewahi kuwa mbunge wa Jimbo la Monduli anatajwa kuwa mmoja wa mahasimu wa kisiasa wa muda mrefu wa Lowassa. Molloiment anasema anamfahamu Lowassa tangu, akiwa mdogo kwa kuwa baba yake alikuwa tarishi ofisi ya Mkuu wa Wilaya. Lowassa amezaliwa hapa Monduli, ameishi hapa, kama binadamu ana mapungufu na mazuri yake na mimi ni mmoja wa watu ninayemjua sana,” anasema.

Anasema miongoni mwa mambo ambayo yanamsababishia Lowassa uadui tangu akiwa mdogo ni kupenda kusimamia mambo ambayo anayaamini, hata kama wenzake hawaungi mkono.

“Tangu kijana alikuwa na misimamo yake, akitaka jambo liwe lazima liwe, na hii ndio sifa yake kubwa ina uzuri na ubaya wake,” anasema.

“Mimi sina kinyongo naye, huyu ni mchapakazi na ana upeo wa mambo mengi tofauti na viongozi wengi tulionao,” anasema Molloiment.

Dada alonga

Kalaine Lowassa, dada yake Edward, aliiambia Mwananchi nyumbani kwake kuwa kaka yake kwa sasa ndio kiongozi wa familia yao kutokana na kifo cha wazazi wao. Kalaine anasema tangu utoto, Edward alikuwa tofauti na wao, alipenda kukaa na wazee na kuzungumza. Anasema hata pale ambapo wao walikuwa na jambo la kumueleza baba yao, walimtuma Edward kumuuliza baba yao au hata kumueleza mambo mbalimbali.

“Edward alikuwa anajiamini sana, ukimtuma jambo zuri kwa wazee, anafikisha na analitetea bila woga,” anasema.

Lowassa alishiriki vita na Uganda

Anasema anakumbuka wakati wa vita kati ya Tanzania na Uganda, Edward aliteuliwa kwenda vitani na kusababisha familia yake kubaki na hofu kubwa hadi aliporejea salama.

“Baba alikuwa anasikiliza redio na jioni anatuelezea jinsi vita inavyoendelea, tulipata hofu kubwa lakini baadaye alirudi. Nakumbuka alirudi na ndevu na alituelezea habari za vita na kututaka tuipende Tanzania,” anasema.

Lowassa aligombea urais kwa mara ya kwanza mwaka 1995.

Advertisement